Jumanne, 21 Agosti 2018

UONGOZI WA MAHAKAMA DODOMA WAFANYA JITIHADA ZA KUPATA MAHAKAMA ZA WILAYA KATIKA WILAYA ZISIZO NA MAHAKAMA KATIKA MKOA HUO


Na Stanslaus Makendi, Mahakama Kuu Dodoma

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma imeanza mpango wa uanzishaji wa huduma za Kimahakama katika Wilaya zisizo na huduma hizo kwa sasa.

Viongozi wa Mahakama katika Kanda hiyo wameanza kufuatilia na kukutana na Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba na Chamwino ili kupata maeneo ambayo yatatumika na Mahakama za Wilaya katika kipindi ambacho mpango wa kujenga Mahakama za Wilaya katika maeneo hayo unafanyiwa kazi.

Utekelezaji huu unafuatia agizo la Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania juu ya kufanya jitihada ya kuwa na Mahakama hizo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Katika mazungumzo waliyofanya katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo ilibainika kuwa huduma ya Kimahakama inahitajika sana kwa sasa katika eneo hilo kutokana na umbali mrefu uliopo kufikia eneo ambalo huduma za Mahakama ya Wilaya inapatikana kwa sasa (Kondoa). 

Baada ya mazungumzo hayo viongozi wote wa pande mbili walitembelea na kuona eneo ambalo Ofisi ya Mkurugenzi imetenga kwa ajili ya matumizi ya Mahakama na Taasisi nyingine muhimu ambazo hazipo kwa sasa katika Wilaya hiyo.

Sambamba na hilo, viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino nao walionesha uhitaji mkubwa wa uanzishaji wa Mahakama ya Wilaya katika eneo hilo na wameahidi kutoa ushirikiano mkubwa ili kuhakikisha huduma hiyo inaanzishwa mapema katika Wilaya hiyo.

 Aidha kwa sasa wanafanya jitihada za kuhakikisha jengo linapatikana ili kuanzisha huduma hiyo muhimu kwa wananchi wa Wilaya ya Chamwino.

Katika zoezi la ufuatiliaji wa suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Wilaya ya Chemba ambayo inahudumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Kondoa kwa sasa, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma Bibi. Maria Francis Itala waliambatana na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mheshimiwa Arnold John Kirekiano walitembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Kondoa ambayo kwa sasa umefikia hatua ya uezekaji wa paa na shughuli za kukamilishwa kwake zikiwa zinaendelea vizuri.

Mahakama ya Tanzania kupitia mpango Mkakati wake wa miaka mitano 2015/2016 – 2019/2020 hususani nguzo ya pili ya mpango mkakati huo inalenga kusogeza huduma za Mahakama kwa wananchi kwa kuhakikisha huduma hizo zinafikika kwa urahisi kwa maeneo yote nchini.
Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma Bi. Maria Francis Itala, (wa pili kushoto) akiwa katika Ofisi ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Chemba kufuatilia upatikanaji wa majengo kwa ajili ya uanzishaji wa Mahakama ya Wilaya ya Chemba.
Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma na Hakimu Mkazi Mfawidhi (M) wakitoka katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba kwa ajili ya kwenda kuona eneo lililopendekezwa kwa ajili ya uanzishaji wa Mahakama ya Wilaya pamoja na kuoneshwa kiwanja cha Mahakama katika Wilaya hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Chemba akionesha eneo la kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Chemba ambalo linapakana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo.
Muonekano wa nje wa jengo lililopendekezwa kwa ajili ya Mahakama ya Wilaya ya Chemba.
Nyumba iliyoombwa kwa ajili ya makazi ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Chemba.


Muonekano wa jengo linalotumika kwa sasa na Mahakama ya Wilaya ya Kondoa ambayo inatoa huduma za kimahakama kwa Wilaya ya Kondoa na Chemba.
Muonekano wa mradi wa ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Kondoa kwa sasa.
Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma (wa pili kushoto) akitoa maelekezo kwa Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Kondoa Bi. Edna Edward Dushi juu ya kuanza zoezi la upandaji wa miti katika eneo hilo ambapo Mahakama ya Wilaya ya Kondoa inayojengwa. 
(Picha na Stanslaus Makendi, Mahakama Kuu Dodoma) 

Maoni 1 :

  1. Hongereni sana Mahakama ya Tanzania kwa jitihada kubwa mnazozifanya kuwapelekea huduma ya upatikanaji wa haki wananchi

    JibuFuta