Ijumaa, 7 Septemba 2018

JAJI KIONGOZI ATAKA KESI ZINAZOHUSU FIDIA KWA WAFANYAKAZI KUSIKIIZWA KWA HARAKA


 Na Victor   Kitauka, Morogoro

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Jaji Dkt. Eliezer M. Feleshi amesema hategemei kuona kesi za fidia kwa wafanyakazi zikicheleweshwa mara zinapofikishwa mahakamani.       

Jaji  Dkt Feleshi ameyasema hayo   wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa mahakimu wakazi wafawidhi kutoka mikoa ya  Dar es salam Pwani, Morogoro,Lindi  na Mtwara.   

Mafunzo hayo ya siku mbili  ambayo yanameandaliwa  na Chuo cha Uongozi wa mahakama Lushoto(IJA) na kuendeshwa na Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi yaliyofanyika katika ukumbi wa NSSF Morogoro kuanzia  Septemba  5  mpaka 6 mwaka ,2018.                              

Akifungua mafunzo hayo Jaji Kiongozi alieleza umuhimu wa mafunzo hayo kwa  mahakimu kuhusu utekelezaji wa sheria hiyo na umuhimu wa kesi hizo kusikilizwa kwa haraka alisema, huduma ya hifadhi ya jamii ni haki inayotambulika na kulindwa na kikatiba kwenye ibara ya 11(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977.

Aliongeza kwamba, wakumbuke  kuwa  kesi hizo zinamhusu mfanyakazi aliyeumia,inagusa uhai,inahusu ulemavu wa kudumu kwa hiyo nyuma kuna wategemezi na yeye mwenyewe kwa hiyo inahusu maisha ya mtu.                   

 “Sitegemei kesi za namna hii ziingie kwenye kundi la njoo kesho,njoo kesho, kesi za namna hii zikiingia zisikilizwe mfululizo kwani ushahidi wake upo wazi na adhabu zake zipo bayana” Alisisitiza  Dk. Feleshi. 

Aidha Dkt Feleshi aliongeza  kwamba  kwa mujibu wa sheria kila mfanyakazi aliyeumia au kuugua kazini ana haki ya kupata fidia stahiki na  kwa wakati na kwa yule atakayefariki kazini basi wategemezi wake wana haki ya  kupata haki zilizoainishwa kisheria.

Akiainisha  sheria hiyo ya mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi unavyofanya  kaziJaji Feleshi alinukuu sheria ya sasa ya Fidia kwa wafanyakazi katika vifungu vya 22(1) 46 na 48 na pia katika  majedwali ya 2,3 na 4,ambapo alisema sheria imeweka bayana kuwa ulipaji wa Fidia unazingatia zaidi uhalisia wa tukio.

Ikiwemo ,kiwango cha hasara na madhara ambayo  mfanyakazi amepata ndio vinafanya fidia inayolipwa ikokotelewe kwa kufuata asilimia ya vigezo hivyo na malipo ya ujira wa mwezi au malipo mwisho ya muhusika. 
Naye Mkurugenzi Mkuu wa  Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Bw. Masha Mshomba kwa upande wake alieleza kuwa  kwa  sasa kipaumbele cha  Mfuko ni kutoa elimu kwa wadau mbalimbali ikiwemo mahakimu ili kuwawezesha kuwa uelewa mpana na  jinsi ya kutekeleza sheria iliyoanzisha.

Alisema  kwa sasa  Mfuko  umeweza kuwafikia wadau wengi na matokeo makubwa yameanza kuonekana kwani kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika uelewa na utekelezaji wa sheria hii.      
Katika Mafunzo hayo Mahakimu wakazi wafawidhi wamejifunza sheria inayosimamiamasuala ya fidia kwa wafanyakazi pia jinsi muundo wa Mfuko wa fidia kwa wafanyakazi ulivyo na taratibu za utoaji  wa  fidia pale mfanyakazi anapopata madhara kazini au kufariki.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Jaji Dkt. Eliezer M. Feleshi  akizungumza jambo  kuhusu Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi katika mafunzo  ya Mahakimu kutoka Dar es Salaam, Pwani,Mtwara Lindi na Morogoro

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Jaji Dkt. Eliezer M. Feleshi  akizungumza jambo  kuhusu Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi(WCF) katika mafunzo  ya Mahakimu kutoka Dar es Salaam, Pwani,Mtwara Lindi na MorogoroKulia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama-Lushoto, Mhe Jaji Dkt. Paul  Khwelo na Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa WCF,Masha Mshomba.  


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Jaji Dkt. Eliezer M. Feleshi  (watatu  kulia )akiwa  katika picha ya pamoja  na baadhi ya  Mahakimu kutoka Dar es Salaam, Pwani,Mtwara Lindi na Morogoro

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni