Alhamisi, 13 Septemba 2018

JAJI MFAWIDHI WA MAHAKAMA KUU TANGA ATEMBELEA OFISI YA MKUU WA WILAYA TANGA


 Na Amina Ahmad, Mahakama Kuu-Tanga

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Amiri Rajabu Mruma ametembelea ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tanga ikiwa ni ziara yake ya kwanza ya kikazi tangu kuhamia Mkoani Tanga.  

Katika ziara hiyo iliyofanyika Septemba 12, 2018, Mhe. Jaji Mfawidhi aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Francis Kabwe, Mtendaji wa Mahakama kuu Kanda ya Tanga, Bw. Ahmed Selemani Ng’eni, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Tanga Mhe. Ruth Mkisi, Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya ya Tanga Bi. Subira Mwishashi na Afisa TEHAMA wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga Bi. Amina Ahmad. 

Akiwa ofisini hapo, Jaji Mruma alipata fursa ya kuzungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tanga na kujadili mambo mbalimbali hususani masuala ya migogoro ya Ardhi na Mirathi, wajibu wa msimamizi wa Mirathi na haki za mjane kwenye mirathi. 

Mkuu wa wilaya ya Tanga, Mhe. Thobias Mwilapwa alimshukuru sana Jaji Mfawidhi kwa kwenda kujitambulisha kwa mara ya kwanza na kutoa elimu ya kutosha kwa wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama. 

Kwakuwa mada alizotoa Jaji Mfawidhi zilionekana ni changamoto kwa Wilaya, kikao kiliazimia kwamba Mahakama kanda ya Tanga ianzishe utaratibu maalum wa kutoa elimu kwa umma kupitia Tanga Televisheni ili wananchi waweze kuelewa haki zao kisheria.

Vituo vingine ambavyo Jaji Mfawidhi alivitembelea ni Ofisi ya Mtendaji wa kata ya Central, ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Pongwe, Mahakama ya Wilaya ya Tanga na Mahakama za mwanzo mjini Tanga, Mwang’ombe na Pongwe.
 Mhe. Jaji Amiri Rajabu Mruma akisaini kitabu cha wageni katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tanga. Katikati ni Naibu Msajili, Mahakama Kuu Tanga, Mhe. Francis Kabwe na kulia ni Mhe. Ruth Mkisi, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Tanga.
Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mhe. Thobias Mwilapwa akifungua kikao rasmi, kushoto ni Jaji Mfawidhi Mhe. Amir Rajabu Mruma akifuatiwa na Naibu Msajili Mhe. Francis Kabwe. Kulia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Tanga Bi. Faidha Salim. 

Jaji Mruma akizungumza na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa Wilaya ya Tanga.

(Picha na Amina Ahmad, Mahakama Kuu, Tanga)



 

 





Maoni 2 :

  1. mungu awasimamie katika majukumu ya utendaji wenu wakazi

    JibuFuta
  2. Kwakweli tanga mahakama ya aridhi aitendi aki sheria watumia kutoka vichwani na kumuofisha mtu na kumnyima aki na akuna pakusemea tunapofeza aki sana tanga naomba msada

    JibuFuta