Ijumaa, 28 Septemba 2018

MAHAKAMA KUU WAJADILI MIKAKATI YA KUMALIZA MASHAURI MAHAKAMANI

Na Lydia Churi
Majaji, Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na divisheni zake wamekutana na kujadili mikakati mbalimbali itakayowezesha mashauri kumalizika kwa haraka na kwa wakati Mahakamani.

Katika kikao kilichoongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi, viongozi hao wa Mahakama walipata nafasi ya kujadili mikakati mbalimbali ya kumaliza kwa wakati mashauri mahakamani ikiwemo kusajili kwa usahihi mashauri yote yanayofunguliwa kwenye mahakama hizo.

Akiwasilisha mada kuhusu hali ya mashauri,  Naibu Msajili Mhe. Shamira Sarwatt aliitaja mikakati mingine itakayosaidia kanda hiyo kumaliza mashauri kwa wakakti kuwa ni kushughulikia mashauri kwa mpangilio wa namna yanavyosajiliwa pamoja na kuwa na program maalum ya kusikiliza na kumaliza mashauri ya muda mrefu yaliyoko mahakamani.
Aidha, mikakati mingine inayoweza kusaidia kumaliza mashauri kwa wakati ni pamoja na matumizi ya Tehama, kutokuahirishwa mara kwa mara kwa mashauri Mahakamani, na kuhakikisha mashauri hayakai muda mrefu na kusababisha mlundikano. Mkakati mwingine ni kushirikiana kwa karibu zaidi na wadau wa Mahakama.

Baadhi ya wadau wa Mahakama ni Polisi, Magereza , Takukuru, na  Ofisi ya Mwanansheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Katiba na Sheria na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
Akizungumza kwenye Mkutano, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliwataka Watendaji wa Mahakama pamoja na Naibu Wasajili kufanya kazi kwa ushirikiano kwa kuwa kila mmoja anamtegemea mwenzake katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku

Alisema endapo Watendaji na Naibu Wasajili watafanya kazi zao kwa ushirikiano ni dhahiri kuwa kasi ya usikilizwaji wa mashauri itaongezeka na hivyo kuondoa mlundikano wa mashauri mahakamani na wananchi watapata haki zao kwa wakati.

 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akizungumza na Majaji wa Mahakama kuu ya Tanzania, Naibu Wasajili pamoja na Watendaji wa Mahakama katika kikao Maalum kujadili mikakati ya kumaliza mashauri Mahakamani kwa wakati kilichofanyika jana jijini Dar es salaam.  

Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa katika kikao Maalum cha kujadili mikakati ya kumaliza mashauri Mahakamani kwa wakati kilichofanyika jana jijini Dar es salaam.  
 
 
Watendaji wa Mahakama pamoja na Naibu Wasajili wakiwa katika kikao Maalum cha kujadili mikakati ya kumaliza mashauri Mahakamani kwa wakati kilichofanyika jana jijini Dar es salaam.  

(Picha na Mary Gwera) 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni