Ijumaa, 28 Septemba 2018

WANANCHI MBEYA WAELIMISHWA KUHUSU MIRATHI NA WOSIA


Na Rajabu Singana-Mahakama Kuu Mbeya

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya Mhe.Dkt. Mary Levira ametoa wito kwa wananchi wa kanda hiyo kuhakikisha wanaandaa ushahidi unaojitosheleza ili wanapofika mahakamani waweze kuhudumiwa kwa wepesi na kupata haki wanazostahili.
Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu kuhusu masuala mbalimbali Mahakamani hapo, Jaji Levira pia amewataka wananchi hao kutokuwa na hofu katika kuandaa wosia kwa kuwa ni njia pekee inayompa nafasi mmiliki wa mali kurithisha watu wanaostahili na anaohitaji warithi mali zake.

Naye Jaji wa Mahakama Kuu kanda ya Mbeya Mhe. Paul Ngwembe pia amewataka wananchi kuzingatia kila kinachofundishwa na wawezeshaji ili kuwa na uelewa mpana zaidi wa masuala ya kisheria.

Alisema asilimia kubwa ya utajiri wa Mwafrika huishia kizazi cha kwanza pekee kutokana na watu wanaorithi mali za marehemu kutumia vibaya mali hizo. Aliwataka wananchi kuitumia vizuri elimu wanayopata ili utajiri wa marehemu uwe endelevu.

Jaji Ngwembe pia aliwatahadharisha wananchi kutokwenda kwa matapeli washeria maarufu kama makanjanja kwa sababu wamekuwa wakichangia katika  upotoshaji wa huduma za  Mahakama.         

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya Mhe.Dkt. Mary Levira akitoa elimu kuhusu masuala ya Urithi, Mirathi na Wosia kwa wananchi.
Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mhe. Michael Mteite naye aliwakumbusha wananchi kuwa wanapofikia maamuzi ya kuandika wosia wahakikishe wosia huo unakidhi taratibu zote za kisheria kama walivyofundishwa na wahakikishe wanafanya siri kubwa catlike wosia huo.
Naye Wakili wa Kujitegemea Mhe. Juliana Marunda aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuanzisha utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi kwa kuwa unawasaidia wananchi kuwa na uelewa wa masuala muhimu ya Kimahakama.



Baadhi  ya wananchi wakimsikiliza Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania   kanda ya Mbeya Mhe.Dkt. Mary Levira  wakati  akitoa elimu kuhusu masuala ya Urithi, Mirathi na Wosia .
Alienda mbali zaidi kwa kukitaka Kituo Jumuishi kuweka matangazo ya mada zitakazofundishwa wiki moja kabla ili wananchi wawe na taarifa. Vilevile alitoa mapendekezo kwa Kituo Jumuishi kutoa nakala za elimu inayofundishwa kama rejea muhimu kwa wananchi.

Wanufaika wa huduma za Kituo Jumuishi pia wameelezea kufurahishwa na elimu hiyo inayotolewa bure kwa kuwa inawajengea ufahamu mkubwa. Akitoa maoni yake Bw. Mtawa Kapalata aliipongeza mahakama kwa elimu nzuri ya mirathi na wosia na kuita kakuendelea kutoa huduma hii zaidi katika masuala mbalimbali ya kimahakama.

“Utaratibu huu ni kama umechelewa sana kwa sababu inawezekana rushwa ili kuwa inatokana na wananchi kutofahamu mambo muhimu ya kimahakama hivyo kupitia program hii itawajengea wananchi uelewa mkubwa kuhusu mambo ya kimahakama na kupelekea kuondoa rushwa mahakamani”, alisema mwananchi huyo.
Kituo Jumuishi cha Utoaji wa Huduma za Mahakama kilichopo Mbeya kimeendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu sheria mbalimbali wanapofika mahakamani ikiwemo masuala ya Urithi, Mirathi na Wosia.

Katika kutekele za Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania(2015/2016-2019/2020), Kituo Jumuishi cha Utoaji wa huduma za Mahakama hutoa Elimu kwa wananchi wanaofika Mahakamani hapo kila siku za Jumanne, Jumatano na Alhamisi ya kila wiki ambapo wiki hii elimu hiyo ilitolewa Septemba25 hadi 27, 2018.
 
 

 
 
 


 
                                   


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni