Jumatatu, 1 Oktoba 2018

MAHAKIMU WA KANDA YA MBEYA WATAKIWA KUTOA HAKI BILA UPENDELEO


Na Rajabu Singana. Mahakama Kuu Mbeya

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Robert  Makaramba amewataka mahakimu wa kanda hiyo  kutambua kuwa wao ni walinzi wa haki na wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao wahakikishe wanatenda haki bila kuzingatia rangi, dini, wala hadhi ya watu wanaowahudumia.
Hayo yalisemwa na Jaji Makaramba mwishoni wiki wakati akifungua mafunzo  ya kuwajengea uwezo mahakimu hao.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Robert Makaramba akiwasilisha mada
“Mfanyeni kazi kwa kuzingatia viapo vyenu. mmeitwa kuhudhuria mafunzo haya  ambayo yawajengee ufahamu mkubwa ili kuhakikisha haki inatolewa kwa wakati na ubora”alisema Jaji huyo. 
Mafunzo yaliyotolewa yalilenga kuwajenga katika maeneo yafuatayo ambayo ni makosa ya mara kwa mara ambayo hufanywa na Mahakimu katika uendeshaji wa mashauri mahakama za chini, mamlaka za kimahakama,mahakama za Mwanzo, Wilaya na Hakimu Mkazi, zikiwemo kanuni mbalimbali za uandishi bora wa hukumu  pamoja na maadili na miiko ya Mahakimu.

Katika mafunzo hayo changamoto mbalimbali ziliweza kuibuliwa na washiriki, kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi. Hivyo washiriki wametakiwa kuweka jitihada kubwa katika kusoma, kuelewa na kuzitafsiri sheria, kanuni na taratibu mbalimbali zinazotumika kuendesha mahakama kwa ngazi husika.

Jaji wa Mahakama Kuu kanda ya Mbeya Mhe. Paul Ngwembe akiwasilisha mada.
Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Watoto Mbeya Mhe. Zawadi Laizer aliwataka Mahakimu wateule wanaosikiliza mashauri ya Watoto wahakikishe wanasoma waraka wa Jaji Mkuu unaoelekeza namna ya kuendesha mashauri ya watoto. Aliongeza kwa kusema hukumu ya mtoto haitakiwi kulenga kumwadhibu bali kumrekebisha mtoto.
Akifunga mafunzo hayo ya siku moja Mwenyekiti wa Kamati ya Mafunzo kanda ya Mbeya, Mhe Dkt. Mary Levira aliwataka washiriki kuyazingatia yote yaliyofundishwa, kuwashukuru kwa ushirikiano na utulivu walioonesha washiriki. Vilevile aliwataka washiriki kujiwekea utaratibu wa kuibua agenda mbalimbali ambazo zitawekwa katika mpango wa mafunzo. 

Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi  wa Mahakama ya Watoto Mbeya Mhe. Zawadi Laizer akiwasilisha mada.


Baadhi ya mahakimu  wa kanda hiyo wakiwa  katika mafunzo hayo.
Naye mwakilishi wa washiriki, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mjini (Mbeya) Mhe. Fadhili Luvinga akitoa neno la shukrani alisema anashukuru kwamafunzo yaliyotolewa na kuuomba uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya kuendelea kutoa mafunzo mbalimbali yatakayosaidia kuwajenga.

 Alisema kuna uhitaji mkubwa wa mafunzo kutokana na Mahakimu wengi kurithi makosa kutoka kwa watangulizi wao katika maeneo yao ya kazi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni