Na
Rajabu Singana, Mahakama Kuu Mbeya
Kituo Jumuishi cha
utoaji huduma za Mahakama Mbeya, kimeanzisha utaratibu wa kuongea na wananchi
wanaofika kwa ajili ya kupata huduma za Mahakama asubuhi kabla kuanza kwa
Mahakama.
TY66O
Akizungumza katika
ufunguzi wa tukio hilo, Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, Mhe. Jaji, Dkt. Mary
Caroline Levira alisema kuwa jitihada hizi zinalenga kuisogeza Mahakama karibu
na kuwajengea imani wananchi juu ya utendaji kazi wa Mhimili huu muhimu.
Aidha; wananchi
walitangaziwa juu ya uwepo wa huduma ya kusambaziwa nyaraka za Mahakama
ijulikanayo kama Posta Mlangoni ambayo hutolewa na Shirika la Posta kwa
kuwapelekea wananchi taarifa za Mahakama popote wanapopatikana.
Mhe. Jaji Levira pia aliwasisitiza
wadau wote wa Mahakama pamoja na wananchi kufanya kazi kwa kushirikiana ili
kufikia dira ya Mahakama isemayo Utoaji wa Huduma kwa Wote na kwa Wakati.
Vilevile wananchi
waliaswa kuwasilisha taarifa zao sahihi pale wanapofika Mahakamani ili kufanya
utekelezaji wa Posta Mlangoni kuwafikia kwa urahisi.
Mbali na hilo, Wananchi
walijulishwa juu ya kuanzishwa kwa Huduma za Kibenki katika jengo hilo.
“Hatua hii inafuatia
mazungumzo yaliyofanyika kati ya uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya na
uongozi wa NMB. Hatua hii ni muhimu kutokana na kuwapunguzia wananchi pamoja na
wadau wengine adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za kibenki. Huduma
hizi zinatolewa kupita Wakala wa NMB ambaye atakuwa akifanya kazi muda wote wa
saa za kazi,” alisema Mhe. Jaji Dkt. Levira.
Kwa ujumla, walipatiwa
elimu kuhusu taratibu mbalimbali za Mahakama pamoja na kukumbushwa juu ya utaratibu
wa mavazi wanayotakiwa kuvaa wanapokuja mahakamani, namna ya kufungua mashauri,
muda wa kukata rufaa, mamlaka za
Mahakama (Mwanzo, Wilaya na Mahakama ya Hakimu Mkazi).
Naye Bw. Masache Kasaka
ambaye ni Afisa TEHAMA aliwaambia wananchi na wadau wa Mahakama juu ya uwepo wa
tovuti ya Mahakama (www.judiciary.go.tz) ambayo kupitia tovuti hiyo wanaweza
kupata fomu mbalimbali zinazoonesha ada za mahakama, kuona na kupakua jarida la
Mahakama ambalo huonesha taarifa mbalimbali.
Utaratibu wa kutoa
elimu utakuwa ukifanywa kila siku za jumanne, jumatano na alhamisi.
Wadau muhimu waliohudhuria
katika uzinduzi wa zoezi hilo ni pamoja na Mawakili wa Serikali, Mawakili wa
Kujitegemea, Polisi, Magereza na wengineo.
Mahakama ya Tanzania
kupitia Mpango Mkakati wake imejiwekea nguzo kuu tatu moja ya nguzo hizo ni ya Kurejesha
imani ya jamii na Ushirikishwaji wa Wadau ambapo kupitia nguzo hii
Mahakama inafanya jitihada mbalimbali ili
wananchi waweze kujua zaidi huduma na maboresho yanayojiri kwa manufaa ya
wananchi kwa kuwa wao ndio wadau wakubwa wa Mhimili huu.
Mbali na Mbeya zoezi la utoaji elimu
kwa wananchi na kuwasikiliza wateja wanaofika katika Mahakama nchini tayari
limeshaanza katika Kanda mbalimbali za Mahakama, ikiwa ni pamoja na Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mwanza, Tabora, Dodoma na kadhalika.
Jaji wa Mahakama Kuu,
Kanda ya Mbeya aliyesimama mbele, Mhe. Jaji Dkt. Mary Caroline Levira akizungumza
wakati wa uzinduzi wa huduma ya utoaji elimu kwa wananchi.
Baadhi ya Watumishi wa
Mahakama Kanda ya Mbeya walioshiriki katika uzinduzi wa utoaji elimu kwa
wananchi wanaofika Mahakama kupata huduma.
Mtendaji wa Mahakama
Kuu, Kanda ya Mbeya, Bw. Moses Mwidete akiongea jambo na Wananchi/Watumishi
waliohudhuria katika hafla hiyo.
Afisa Tehama, Mahakama
Kuu, Kanda ya Mbeya, Bw. Masache Kasaka akitoa elimu kuhusu TEHAMA Mahakamani.
Muonekano
wa Ofisi ya kutoa huduma za kibenki iliyopo ndani ya jengo la Mahakama Kuu,
Kanda ya Mbeya.
(Picha
na Rajab Singana, Mahakama Kuu, Mbeya)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni