Na Mary Gwera, Mahakama
JAJI Kiongozi, Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amewahakikishia Majaji Wastaafu kuwa
Mahakama itaendelea kushirikiana nao katika masuala mbalimbali licha ya kuwa
wamemaliza muda wao wa kazi.
Mhe. Jaji Feleshi
aliyasema hayo, Septemba 22 jijini Dar es Salaam, katika hafla fupi ya kuwaaga jumla
ya Majaji Wastaafu tisa (9) kutoka Mahakama Kuu- Masjala Kuu, Kanda ya Dar es
Salaam, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi na Kazi.
“Napenda kuwapongeza
kwa Utumishi wenu uliotukuka kwa Mahakama hadi kufikia siku ya leo, nipende
kuwahakikishia kuwa Mahakama itaendelea kuwa pamoja nanyi kwa kila hali, iwe
kwa shida au raha,” alisema Jaji Kiongozi.
Aidha; Mhe. Jaji
Kiongozi aliwataka Majaji hao kutosita kushiriki katika shughuli mbalimbali za Mahakama
ili kuendeleza maboresho ambayo Mahakama inakusudia kufikia kupitia Mpango
Mkakati wake.
Aliongeza kwa kuwasihi
Majaji hao Wastaafu kutosita kutoa ujuzi wao kwa Majaji ambao bado wapo kwenye Utumishi wa
Umma pindi wanapohitajika kutoa elimu katika Mafunzo mbalimbali yanayofanyika
ndani ya Mahakama.
Kwa upande wake, Jaji
Mstaafu, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Fredrica Mgaya ameushukuru
Uongozi wa Mahakama kwa kuwaandalia hafla hiyo kwani wamefurahi na kujisikia
kuwa wao bado ni sehemu ya Wanafamilia wa Mahakama.
Kwa ujumla Majaji hao
Wastaafu kila mmoja kwa nafasi yake waliishukuru Mahakama ya Tanzania kwa
kuwalea na kufanya kazi kwa ushirikiano katika kipindi chote cha utumishi wao.
Vilevile wametoa wito
kwa Watumishi wa Mahakama ambao bado wapo kazini kufanya kazi kwa bidii na
kupenda kazi zao.
Majaji Wastaafu walioagwa
ni pamoja na Mhe. Sekieth Kihio, Mhe. Projestus Rugazia, Mhe. Augustine
Shangwa, Mhe. Laurence Kaduri, Mhe. Gadi Mjemmas, Mhe. Fredrica Mgaya, Mhe. Ibrahim
Mipawa, Mhe. Aghaton Nchimbi, na Mhe. Pelagia Khaday.
Jaji Kiongozi, Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akitoa neno wakati wa hafla ya
kuwaaga rasmi Majaji Wastaafu wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam,
walioketi ni sehemu ya Majaji Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam pamoja na
Divisheni walioshiriki katika hafla hiyo.
Jaji Mstaafu wa
Mahakama Kuu, Mhe. Sekieth Kihio akipokea zawadi kutoka kwa Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi, (katikati) ni Jaji wa
Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Jaji Munisi.
Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akimpatia zawadi, Jaji
Mstaafu Mhe. Laurence Kaduri ikiwa ni ishara ya pongezi kwa kumaliza utumishi
wa Mahakama salama.
Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akimpatia zawadi,
Mhe.
Jaji Mstaafu Gadi Mjemmas.
Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akimpatia zawadi,
Mhe.
Jaji Mstaafu Fredrica Mgaya.
Jaji Mstaafu wa
Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, Mhe. Ibrahim Mipawa akitoa neno la shukrani.
Jaji Kiongozi, Mhe.
Dkt. Eliezer Feleshi (katikati) pamoja na baadhi ya Majaji wengine wa Mahakama Kuu
waliohudhuria katika hafla wakiwa katika picha ya pamoja na Majaji Wastaafu, wa
kwanza kushoto ni Jaji Mstaafu, Mhe. Sekieth Kihio, wa pili kushoto ni Jaji
Mstaafu, Mhe. Laurence Kaduri, wa pili kulia ni Jaji Mstaafu, Mhe. Fredrica
Mgaya, wa kwanza kulia ni Jaji Mstaafu, Mhe. Ibrahim Mipawa. Waliosimama wa
pili kulia ni Jaji Mstaafu, Mhe. Gadi Mjemmas, wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Beatrice Mutungi, wa kwanza
kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Jaji Munisi na wa
kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Ilvin
Mugeta.
Jaji Kiongozi, Mhe.
Dkt. Eliezer Feleshi (katikati) pamoja na baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu
waliohudhuria katika hafla ya kuwaaga Majaji Wastaafu wakiwa katika picha ya
pamoja na Majaji hao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni