Na
Amina Ahmad, Mahakama Kuu, Tanga
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Amir Mruma amemuhimiza Mkandarasi SUMA JKT
kuharakisha ukamilishaji wa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Magoma iliyopo Wilayani
Korogwe ili ianze kutumika mara moja.
Akiwa katika ziara ya
kikazi Wilayani Korogwe; Mhe. Jaji Mruma
alipata fursa ya kutembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mahakama hiyo Oktoba
23 ambapo hata hivyo aliridhishwa na hatua iliyofikiwa.
Katika ziara yake
Wilayani humo, Mhe. Jaji Mfawidhi alifanikiwa pia kukutana na Kamati za
Maendeleo za Kata ya Magoma na Mashewa na kutoa elimu juu ya haki na wajibu wa wananchi katika migogoro ya
ardhi, kesi za ubakaji, mimba za utotoni na usimamizi wa Mirathi.
Kwa upande wao; Wajumbe
wa Kamati za Maendeleo (WDC) walitoa shukrani zao za dhati kwa Jaji Mfawidhi
kwani ilikuwa ni mara yao ya kwanza kukutana na Jaji na kupewa elimu ya
kisheria, hali iliyowapelekea kumuomba Jaji Mfawidhi aendelee na utarabu wa
kukutana nao mara kwa mara kuwajengea wigo na uelewa mpana wa masuala ya
kisheria ili kufanikisha majukumu yao.
Sambamba na hilo,
wajumbe hao walipongeza pia huduma zinazotolewa na Watumishi wa Mahakama na
kukiri kwamba hakuna malalamiko yoyote juu ya huduma za Mahakama katika vituo
vyao.
Mhe. Jaji Mruma
anatarajia kuendelea na ziara hiyo kwa kuongea na Kamati ya Ulinzi na Usalama
ya Wilaya ya Korogwe, kukagua Mahakama ya Wilaya Korogwe, Mahakama za Mwanzo
Old Korogwe, Manundu, Bungu na Vugiri.
Vilevile atazungumza na
Watumishi wa Mahakama hizo, Kamati za maendeleo za Kata zilizomo Mahakama
husika pamoja na wafungwa na Mahabusu wa Gereza la Manundu na Gereza la
kilimo Kwa Mgumi lengo likiwa ni
kuboresha huduma ya utoaji haki kwa ujumla.
Muonekano wa jengo la
Mahakama ya Mwanzo Magoma lililopo katika hatua za mwisho za ujenzi.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Amiri Rajabu Mruma (kushoto) akipokea maelezo
kutoka kwa Fundi wa Kampuni ya SUMA JKT alipokuwa akikagua ujenzi wa jengo la
Mahakama ya Mwanzo Magoma Wilayani Korogwe.
Mhe. Jaji Mruma akiendelea na ukaguzi.
Jaji Mruma akitoa elimu
kwa Wajumbe wa Kamati ya maendeleo ya Kata ya Hale Wilayani Korogwe.
Mhe. Jaji Mruma (wa
tano kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya maendeleo ya
kata ya Hale. Mstari wa kwanza kulia ni Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya ya
Korogwe, Bw. Emmanuel Machimo akifuatiwa na Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya
Tanga, Bw.Ahmed Ng’eni.
(Picha na Amina Ahmad,
Mahakama Kuu, Tanga)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni