Na
Catherine Francis, Mahakama Kuu Arusha
Jaji Mfawidhi, Mahakama
Kuu- Kanda ya Arusha, Mhe. Mosses Mzuna, amewakumbusha Mahakimu kutekeleza wajibu
wao ipasavyo ili kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mwananchi na kwa wakati.
Akiwa ziarani Mahakama
ya Wilaya Mbulu, Oktoba 23, Mhe. Jaji Mzuna aliwakumbusha Mahakimu wilayani humo kuwa
wanapaswa kutoa adhabu kwa kuzingatia ukubwa wa kosa lenyewe na si kwa
kuhamasishwa na hisia juu ya kesi husika.
“Wajibu wa kila Hakimu ni kuhakikisha haki inatendeka na kupitia mwenendo wa shauri
na maamuzi yaliyotolewa kabla hawajaruhusu jalada kwenda kwenye ngazi nyingine
za Mahakama,” alisistiza Mhe. Mzuna.
Aidha; Mhe. Jaji Mfawidhi alisisitiza juu ya
umuhimu wa taarifa za mashauri kufikia wadaawa
kwa wakati unaostahili ambapo mwenendo wa shauri pamoja na nakala ya
hukumu vinatakiwa viwafikie wadaawa kwa wakati.
Mhe. Mzuna alisema
endapo taarifa hizi zitawafikia Wadaawa mapema zinawawezesha kufanya hatua
nyingine kama watakuwa hawajaridhishwa na maamuzi ya Mahakama hiyo.
Katika kusititiza hilo
Mheshimiwa Jaji Mzuna alifanya ukaguzi mdogo wa majalada ya mashauri
yaliyokamilika ili kuweza kugundua ni kwa jinsi gani Mahakimu wamekuwa
wakitekeleza wajibu wao.
Ukaguzi huo ulihusisha
majalada ya Mahakama ya Wilaya Mbulu na majalada ya Mahakama ya mwanzo
Endagikot. Pia aliwapa maelekezo na mapendekezo pale alipogundua kuna
changamoto katika kutekeleza wajibu wao.
Katika ziara hiyo, Mhe.
Jaji Mfawidhi alikutana pia na Wazee wa Baraza wa Wilaya ya Mbulu ili kuweza
kuwafahamu na kujua changamoto wanazokabiliana nazo ambazo zinakwamisha ufanisi
wa kazi zao.
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Mosses Mzuna (wa kwanza kushoto) akikagua majalada ya
Mahakama ya Mwanzo ya Endagikot iliyopo Wilayani Mbulu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni