Na Rajabu Singana, Mahakama Kuu -Mbeya
Mawakili wa Kujitegemea
Mkoani Mbeya wamepatiwa Mafunzo ya Ushahidi wa Kisayansi ili kuhakikisha huduma
wazitoazo zinawasaidia wananchi ipasavyo katika utatuzi wa matatizo ya kisheria na
uwakilishi Mahakamani .
Akitoa Mafunzo hayo
Oktoba 20, Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu -Kanda ya Mbeya Mhe. Robert Makaramba alisema
Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo wa namna ya kukusanya, kutoa na kuweka
pingamizi Mahakamani hususani katika ushahidi wa kisayansi.
Katika mafunzo hayo,
Mhe. Jaji Makaramba aliwaeleza Mawakili hao kuwa mara
nyingi ushahidi wa kisayansi hutumika kwenye makosa ya jinai ambapo katika
mashauri hayo wataalamu waliobobea katika taaluma husika hutakiwa
kuithibitishia Mahakama kwa kutumia utaalamu wao kuhusiana na tuhuma zilizo
mbele ya Mahakama.
Aidha; Mhe. Jaji
Mfawidhi aliwataka Mawakili hao wanapokuwa wanasimamia mashauri yanayohitaji ushahidi
wa kisayansi kuhakikisha wanapeleka Wataalamu waliobobea katika taaluma husika.
Kwa upande wake, Wakili
wa Kujitegemea, Mhe. Simon Mwakolo aliyezungumza kwa niaba ya wenzake aliishukuru
Mahakama na kusema kuwa mafunzo hayo yametolewa kwa wakati muafaka kwani
mawakili wengi walikuwa hawana ufahamu juu ya namna bora ya kushughulika na
ushahidi wa kisayansi.
Mhe. Mwakolo aliendelea
kusema kuwa kwa sasa watakuwa na uwezo mkubwa wa kukusanya, kuandaa na kuweka
pingamizi za kisheria ili wananchi wanaowasaidia wapate haki zao inavyostahili.
Baada ya marekebisho ya
Sheria ya Ushahidi ya mwaka 1967 kutambua ushahidi wa kisayansi yaliyopelekea
sheria mbalimbali kutungwa na zingine kufanyiwa marekebisho ili kukidhi
matakwa.
Baadhi ya sheria ambazo huhitaji ushahidi wa
kisayansi ni pamoja na Sheria ya Makosa
ya Mitandaoni ya mwaka 2015, Sheria ya
Vinasaba vya Binadamu Namba 8 ya mwaka 2009, Sheria ya Wanyamapori ya mwaka
2009, Sheria ya Utafiti wa Kimahakama juu ya Vifo vyenye Utata namba 24 ya
mwaka 1980 pamoja na Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ya mwaka 2007.
Jaji Mfawidhi, Mahakama
Kuu- Kanda ya Mbeya, Mhe. Robert Makaramba akiwasilisha mada.
Baadhi ya washiriki
wakimsikiliza Mhe. Jaji Makaramba alipokuwa akitoa Mada husika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni