Na
Francisca Romanus, Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma-Mara
Chama cha Ushirika cha
Akiba na Mikopo cha Mahakama kimetoa semina fupi kwa Watumishi wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Musoma pamoja na wa Mahakama ya Wilaya Musoma juu ya shughuli na
umuhimu wa chama hicho kwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania.
Akitoa semina hiyo hivi
karibuni, Katibu wa Chama hicho, Bi. Doris Mwamasage Chama hicho kina madhumuni
mengi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu juu ya mambo mbalimbali ya kijami,
mazingira, kutoa mikopo yenye riba nafuu, kuwajengea wanachama tabia ya kuweka
akiba na amana mara kwa mara, kukopa kwa busara na kulipa kwa wakati, kuepuka
matumizi yasiyo ya lazima n.k
“Pamoja na madhumuni
mengi yaliyopo katika chama, lakini kubwa zaidi ni kutoa huduma za kifedha kwa
wanachama ili waweze kukidhi mahitaji mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kuinua
hali ya maisha yao,” alisema Bi. Mwamasage.
Pamoja na madhumuni
hayo, Bi Doris pia alisema kuwa Chama hiki kimekuwa msaada mkubwa sana kwa watumishi
wanapokumbwa na majanga mbalimbali na hasa kwa watumishi wanaokaribia kustaafu,
kwani akiba na amana zao walizokuwa wakijiwekea zimewasaidia sana kuendesha
maisha yao baada ya kustaafu wakati wakiwa wanasubiri taratibu za malipo yao ya
pensheni kukamilika.
Bi. Mwamasage, aliwaomba
watumishi wa Mahakama kujiunga kwa wingi ili kupata faida mbalimbali ikiwa ni
pamoja na mikopo yenye riba nafuu.
Hata hivyo; Watumishi
waliopata nafasi ya kushiriki katika semina hiyo, waliupongeza Uongozi wa Chama
hicho kwa kuweza kuwaletea mjumbe ambae ametoa elimu juu ya chama hicho ambapo
wengi walikiri hawakuwa na uelewa nacho.
Aidha; Watumishi waliahidi
kujiunga kwani waliona kuwa Chama hicho ni mkombozi kwao, vilevile walishauri
elimu hii pia itolewe na kwingine ili Watumishi waweze kufaidika na Chama
hicho.
Kwa mujibu wa Katibu
huyo, Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Mahakama kilianzishwa rasmi
Januari 08, 1970 na ofisi zake zinapatikana katika Mahakama ya Biashara mkoani Dar
es Salaam.
Katibu wa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Mahakama, Bi
Doris Mwamasage, akitoa elimu juu ya chama hicho kwa Watumishi, kulia ni Afisa
Tawala, Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma Bw, Kandana Lucas.
Baadhi
ya Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma na Mahakama ya Wilaya Musoma
wakisikiliza kwa makini elimu inayotolewa.
Baadhi ya watumishi wakijaza
fomu za kujiunga katika Chama hicho.
(Picha na Francisca Romanus, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Musoma-Mara)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni