Alhamisi, 18 Oktoba 2018

JAMII YASHAURIWA KUJIFUNZA MASUALA YA SHERIA

Na Lydia Churi- Mahakama, Mwanza

Jamii imeshauriwa kujifunza kuhusu sheria ili iwe na uelewa wa masuala hayo kwa kuwa maisha ya binadamu kwa kiasi kikubwa  yanaratibiwa na sheria, kanuni na taratibu.
Kauli hiyo imetolewa leo na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Lake iliyopo jijini Mwanza alipowatembelea kuzungumza nao kuhusu masuala ya maadili na Mahakama.

Mahakama ya Tanzania imeanzisha mpango maalum wa kuzitembelea shule mbalimbali za sekondari pamoja na vyuo ili kuzungumza na wanafunzi kwa lengo la kuwaandaa kuwa na maadili mema katika jamii.
Akizungumza na wanafunzi hao, Jaji Mkuu alisema endapo baadhi ya wanafunzi watataka kuwa wanasheria hapo baadaye hawana budi kuwa na maadili mema kwa kuwa kazi ya utoaji haki  ni ya msingi na inahitaji mtu kuwa na weledi wa hali ya juu.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, licha ya mtu kutokuwa Mwanansheria bado jamii inapaswa kufahamu mambo ya msingi kuhusu sheria kwa kuwa utawala wa sheria msingi wake huanzia nyumbani, kwenye maeneo ya kazi na maeneo mengine na pia sheria, kanuni na taratibu huisaidia jamii kuishi kwa amani.
Alisema mtu kusomea fani nyingine nje ya sheria hakumzuii kujifunza mambo ya msingi kuhusu sheria. “Katika jamii hakuna fani bora kuliko nyingine, ukielewa fani zaidi ya moja unakuwa kwenye nafasi nzuri hasa katika karne hii ya 21 ambayo ili kuendelea ni muhimu fani zote kushirikiana”, alisema Jaji Mkuu.    

Jaji Mkuu aliwashauri wanafunzi hao pia kujifunza mambo ya msingi ili waweze kuendana na karne ya 21 yenye ushindani mkubwa. Aliwataka kujifunza kuhusu teknolojia pamoja na kusoma na kuifahamu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ili wafahamu nchi yao inapokwenda.
Akizungumzia Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Juma alisema inakabiliwa na changamoto nyingi katika utoaji wa haki. Baadhi ya changamoto hizo ni  haki kutokupatikana kwa wakati, upungufu na uchakavu wa baadhi ya majengo ya Mahakama, pamoja na wananchi wengi kutokufahamu sheria na taratibu za kimahakama.

Alisema licha ya kuwapo kwa changamoto hizo, Mahakama hivi sasa iko katika maboresho ya huduma zake kupitia Mpango Mkakati wa miaka mitano ambao unalenga kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi kwa kujenga majengo ya Mahakama, kumaliza mashauri kwa wakati, na kuwaelimisha wananchi kuhusu sheria na taratibu za kimahakama.
Mahakama ya Tanzania hivi sasa inaendelea na ujenzi wa majengo mapya ambapo hadi kufikia mwezi Juni mwaka 2019 jumla ya majengo 52 ya Mahakama yatakuwa yamekamilika kwenye maeneo mbalimbali nchini yakiwemo yale ya Mahakama za Mwanzo, Wilaya, Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama Kuu.

Jaji Mkuu leo amehitimisha ziara yake ya siku nne katika mkoa wa Mwanza ambapo amefanikiwa kutembelea baadhi ya Mahakama zilizopo Ukerewe, Sengerema, Kwimba na Mwanza mjini na kukagua shughuli za Mahakama pamoja na kuzungumza na wafanyakazi. Jaji Mkuu pia alitembelea shule mbili za sekondari za Nyampulukano Sengerema na Lake ya jijini Mwanza.
 Wanafunzi wa shule ya sekondari Lake pamoja na Waalimu wao wakiimba wimbo wa Taifa mara baada ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kuwasili shuleni hapo kwa ajili ya kuzungumza na wanafunzi kuhusu Maadili. 
 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na wananfunzi wa Lake sekondari kuhusu Maadili. Wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mwanza Mhe. Sam Rumanyika na wa kwanza kushoto ni Jaji wa Kanda ya Mwanza Mhe. Mohamed Gwae na wa kwanza kulia ni Jaji wa kanda hiyo Mhe. Agnes Bukuku.
 Baadhi ya Watumishi wa Mahakama wakiimba wimbo wa Taifa walipokuwa katika shule ya sekondari Lake ya jijini Mwanza.
 

  Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati), Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mwanza Mhe. Sam Rumanyika wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mahakama pamoja na wa shule ya Sekondari Lake ya jijini Mwanza mara baada ya Mhe. Jaji Mkuu kuzungumza na wanafunzi wa shule hiyo.

Wanafunzi wa shule ya sekondari Lake wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni