Na
Mary Gwera, Mahakama
Mahakama ya Tanzania
imesema inathamini mchango wa Majaji na Watumishi wengine wa Mhimili huo wanaomaliza
muda wao wa Utumishi kwa mujibu wa Sheria.
Akizungumza na Vyombo
vya Habari baada ya kuwaaga rasmi Majaji Wastaafu wa Mahakama Kuu, Divisheni ya
Ardhi, mapema Oktoba 19,Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt.
Eliezer Feleshi alisema kwa kuzingatia umuhimu huo Mahakama ina utaratibu
maalum wa kuwaaga kitaaluma.
“Mahakama ya Tanzania
inaendelea kujenga umoja, kwa kutambua hili tunatambua kazi nzuri waliofanya
Wastaafu na kuthamini mchango wao katika jukumu zima la utoaji haki nchini,” alisema
Mhe. Jaji Kiongozi.
Aidha; Mhe. Jaji
Kiongozi aliongeza kwa kutoa wito kwa Wananchi kuiamini Mahakama kwani ipo
kuhakikisha inawahudumia kwa kutoa haki kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, mmoja
wa Majaji Wastaafu, Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agathon Nchimbi
aliwaasa Majaji na Watumishi wote wa Mahakama kwa ujumla kufanya kazi kwa bidii
na kwa uadilifu.
“Namshukuru Mwenyezi
Mungu, kwa kunipa nafasi ya kuitumikia Mahakama katika jukumu zito na nyeti la
utoaji haki, wito wangu kwa Watumishi wenzangu waliobaki ni kutekeleza majukumu
yao kwa uadilifu,” alisisitiza, Mhe. Jaji Mstaafu Nchimbi.
Mbali na Mhe. Nchimbi,
Jaji Mstaafu mwingine aliyeagwa katika hafla hiyo ni Mhe. Jaji Gad Mjemmas,
Majaji wengine ambao wamestaafu kutoka Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi ni
pamoja na Mhe. Jaji Projest Rugazia na Mhe. Jaji Fredrica Mgaya.
Hafla hiyo iliyofanyika
katika Ukumbi namba moja (1) wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam
ilihudhuriwa na wageni kadhaa ikiwa ni pamoja na Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Manaibu
Wasajili, Watendaji na baadhi ya Watumishi wa Mahakama.
Jaji
Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (katikati) akiwa
katika hafla ya kuwaaga rasmi Kitaaluma Majaji Wastaafu wa Mahakama Kuu,
Divisheni ya Ardhi, kulia ni Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi,
Mhe. Gad Mjemmas.
Pichani
ni sehemu ya Wahe. Majaji wa Mahakama Kuu, Dar es Salaam waliojumuika pamoja na
Mhe. Jaji Kiongozi na Watumishi na Wageni waalikwa kuwaaga rasmi Kitaaluma
Majaji Wastaafu wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi.
Pichani
ni Jaji Mstaafu, Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Gad Mjemmas akitoa neno
la shukrani katika hafla hiyo.
Naibu
Msajili Mwandamizi, Mahakama Kuu, Mhe. John Chaba (kushoto) akiwa katika hafla
hiyo, kulia ni Naibu Msajili, Mahakama Kuu, Kitengo cha Usuluhishi, Mhe. Saidi
Ding’ohi.
Mwakilishi
kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Bw. Mark Mlwambo akitoa neno katika hafla
hiyo, kulia ni Mwakilishi kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dkt.
Rugemeleza.
Sehemu
ya Maafisa wa Mahakama, Manaibu Wasajili, Watendaji pamoja na Watumishi na
Wageni waalikwa waliojumuika katika hafla hiyo iliyofanyika mapema Oktoba
19,2018 katika Ukumbi namba moja (1) wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.
Pichani
ni baadhi ya Waandishi wa Habari pamoja na Watumishi na Wageni waalikwa
wakifuatilia kwa makini kinachojiri katika hafla hiyo.
Jaji
Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (katikati) akiwa
katika picha ya pamoja na Majaji Wastaafu na baadhi ya Majaji walioshiriki
katika hafla ya kuwaaga Kitaaluma Majaji waliostaafu. Wa pili kushoto ni Jaji
Mstaafu, Mhe. Agathon Nchimbi, wa pili kulia ni Jaji Mstaafu, Mhe. Gad Mjemmas,
wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Crencensia
Makuru na wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi,
Mhe. Rehema Kerefu.
Mhe.
Jaji Kiongozi (katikati) akimkabidhi shada la maua, Jaji Mstaafu, Mhe. Jaji Agathon
Nchimbi ikiwa ni ishara ya pongezi kwa kumaliza muda wa kazi/kustaafu salama
kwa mujibu wa sheria.
Mhe.
Jaji Kiongozi (katikati) akimkabidhi shada la maua, Jaji Mstaafu, Mhe. Jaji Gad
Mjemmas ikiwa ni ishara ya pongezi kwa kustaafu salama, anayeshuhudia
(aliyesimama nyuma mwenye miwani) ni Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kitengo cha
Usuluhishi ‘Mediation’, Mhe. Rose Teemba na kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu,
Divisheni ya Ardhi, Mhe. Crencensia Makuru.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni