Na Rajabu Singana,
Mahakama Kuu Mbeya
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu-Kanda ya Mbeya, Mhe. Robert Makaramba amewaasa Watumishi wa
Mahakama ya Wilaya Rungwe kuwa na mahusiano mazuri katika ufanyaji kazi kwa
kuwa muda mwingi wanautumia wakiwa katika maeneo ya kazi kuliko sehemu
nyingine.
Akiwa katika ziara ya
kikazi katika Mahakama ya Wilaya hiyo Oktoba 19, 2018, Mhe. Jaji Makaramba alifanya
mazungumzo na watumishi wa wilaya hiyo na kuwataka Watumishi hao kufanya kazi
kwa kushirikiana kama timu.
“Tunataka Mahakama safi
na yenye watu safi sio usafi wa suti pekee. Na mnatakiwa kufanya kazi kama
hakuna kesho,” alisema Jaji Mfawidhi huyo.
Mbali na kuzungumza na
Watumishi katika ziara yake, Mhe. Jaji Makaramba alifanya ukaguzi wa ujenzi wa
jengo la Mahakama ya Wilaya Rungwe ambalo linajengwa na Kampuni ya Moladi
Tanzania Limited.
Ujenzi huo unafuatia
jitihada zinazoendelea kufanywa na Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati
wa miaka mitano (2015/2016-2019/2020).
Akitoa taarifa ya
ujenzi huo, Mwakilishi wa Mkandarasi, Mhandisi Erick Muro alisema ujenzi huo
unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Katika hatua nyingine
ili kujenga mahusiano mazuri ya kitaasisi, Mhe. Makaramba alimtembelea Mkuu wa
Wilaya ya Rungwe Mhe. Chalya Julius na kufanya nae mazungumzo.
Mhe. Makaramba alitoa
shukrani kwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kuipatia Mahakama jengo la
kuendeshea shughuli zake kwa muda mrefu. Mazungumzo yao yaligusia uboreshaji wa Kamati ya Maadili ya Mahakimu
ambayo ipo chini ya Mkuu wa Wilaya na walikubaliana kuandaa semina elekezi
itakayohusu namna bora ya kushughulikia maadili ya Mahakimu.
Mhandisi Erick Muro
(mwenye fulana nyeusi) akimuelekeza jambo Mhe. Robert Makaramba alipokuwa akikagua ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Rungwe.
Muonekano
wa jengo la Mahakama ya Wilaya Rungwe linaloendelea kujengwa.
Baadhi
ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Rungwe, wakimsikiliza Jaji Mfawidhi,
Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, Mhe. Robert Makaramba (hayupo pichani) alipokuwa
akizungumza nao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni