Jumatatu, 22 Oktoba 2018

ZIDISHENI MATUMIZI YA TEHAMA MAHAKAMANI: JAJI MZUNA


Na Catherine Francis, Mahakama  Kuu Arusha

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu- Kanda ya Arusha, Mhe. Mosses Mzuna amewakumbusha Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Ngorongoro kuongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA.

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mwishoni mwa wiki iliyopita, Mhe. Jaji Mfawidhi alisema kuwa kipindi hiki cha mabadiliko ya Mahakama ya kutumia TEHAMA watumishi wanalazimika kujifunza na kuelewa matumizi hayo ili kuendana na azma iliyokusudiwa. 

Mhe. Jaji Mzuna alitoa mfano juu ya Mfumo wa kusajili mashauri wa Kieletroniki ujulikanao kama JSDS II kuwa ni muhimu watumishi wote kuufahamu ili waweze kwenda sawa na kasi ya mabadiliko hayo.

Mbali na matumizi ya TEHAMA; Mhe. Jaji Mfawidhi aliongeza kwa kuwaasa Watumishi hao kufanya kazi kwa umoja na bidii ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma iliyo bora zaidi.

 “Msijihusishe na vitendo vya rushwa kwani vinaharibu Taasisi na pia vitawaharibia maisha yenu, mnachotakiwa kuzingatia ni maadili ya kazi kwa muda wote muwapo eneo la kazi na kutumia lugha nzuri pindi mnapohudumia wateja,” alisisitiza Mhe. Jaji Mzuna.

Katika ziara hiyo alipata taarifa ya kiutendaji wa Mahakama hizo kutoka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mhe. Demetrio Nyakunga. 

Aidha; Mhe. Jaji Mzuna alipata nafasi ya kutembelea Mahakama ya Mwanzo Waso Loliondo, Mahakama ya Wilaya Longido, Mahakama ya Mwanzo Namanga na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la Mahakama ya wilaya ya Longido.

Katika ziara yake, Mhe. Jaji Mfawidhi aliambatana na Watendaji wengine wa Mahakama Kanda ya Arusha, lengo likiwa ni kujitambulisha kwa watumishi  na kujua mazingira ya  Mahakama zote zilizopo ndani ya kanda ya Arusha.
 

Jaji Mfawidhi-Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Mosses Mzuna  (aliyesimama) akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Ngorongoro (hawapo pichani).
 
 Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ngorongoro,  Mhe. Demetrio Nyakunga  akisoma taarifa ya utendaji wa Mahakama hiyo mbele ya Mhe. Jaji Mfawidhi.
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha,  Mhe. Mosses Mzuna na Viongozi wa Mahakama, Kanda ya Arusha wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya-Ngorongoro. Wa pili kushoto ni Naibu Msajili Mahakama kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Seif Kulita, wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, wa pili kulia ni Mtendaji,  Mahakama kuu, Kanda ya Arusha, Bw. Edward Mbara na wa kwanza kulia ni Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Ngorongoro, Mhe. Demetrio Nyakunga.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya wilaya Longido, Mhe. Aziza Temu (wa pili kulia) akimuonesha kitu Mhe. Jaji Mfawidhi wakiwa katika jengo la Mahakama la Wilaya Longido linaloendelea kujengwa.
 Muonekano wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Longido lililopo katika ujenzi.

Mhe. Jaji Mzuna akisalimiana na watumishi wa Mahakama ya mwanzo Namanga.

Mhe. Jaji Mzuna akionyeshwa mipaka ya kiwanja cha Mahakama ya mwanzo Namanga.
 (Picha na Benson Fute-Mahakama ya Wilaya, Ngorongoro)

 



 







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni