Na Aisha Abdallah, Mahakama Kuu Tabora
Jaji
Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora, Mhe. Salvatory Bongole amefungua rasmi
Mafunzo ya Mahakimu na Wajumbe wa Mabaraza ya Kata mkoani humo yanayolenga
kuwajengea uwezo wa kuyasimamia mabaraza ya kata katika utekelezaji wa majukumu
kwa mujibu wa sheria.
Akifungua Mafunzo hayo mapema Oktoba 08,
katika Ukumbi wa Katibu Tawala, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Jaji Bongole aliwaelezea
washiriki kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa sababu yataleta uelewa wa pamoja
kati ya Mahakama na Mabaraza ya Kata juu ya mamlaka ya Mahakama na Mabaraza
katika utoaji haki.
Aidha katika hotuba yake ya ufunguzi, Mhe. Jaji Mfawidhi alisisitiza
pia kuhusu umuhimu wa kumsikiliza mtu/mteja kabla ya kutoa maamuzi na kuwaasa wanasemina
kuyatekeleza mambo yote watakayojifunza katika semina hiyo.
“Kama sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati
wa Mahakama suala la ushirikishwaji wa Wadau limepewa kipaumbele ili tuweze
kufanikisha huduma ya utoaji haki”, alisema Mhe. Jaji Bongole.
Katika semina hiyo, Mahakama imewashirikisha
Wanasheria kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora na Halmashauri ya
Manispaa-Tabora kama viongozi wa Mabaraza ya Kata.
Mafunzo hayo ya siku tatu yameandaliwa na Mahakama
ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
Washiriki ni Mahakimu wa Mahakama
za Mwanzo kutoka Tabora Mjini, Urambo, Nzega na Igunga pamoja na wajumbe wa
Mabaraza ya Kata na Wanasheria wa Halmashauri ya Manispaa na wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Tabora.
Sehemu ya Washiriki wakiwa katika Mafunzo hayo.
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda
ya Tabora, Mhe. Salvatory Bongole (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya
pamoja na baadhi ya Mahakimu na Wajumbe wa Mabaraza ya Kata wanaoshiriki katika
Mafunzo ya siku tatu, Oktoba 08, 2018 hadi Oktoba, 10, 2018.
Wengine walioketi wa kwanza kulia
ni Mkurugenzi wa Sheria kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Bw.
Justus Mulokozi, wa pili kulia ni Naibu Msajili Mfawidhi-Mahakama Kuu, Kanda ya
Tabora, Mhe. Hussein Mushi, wa kwanza kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu,
Kanda ya Tabora, Bw. Sumera Manoti, na wa pili kushoto ni Mkufunzi kutoka Chuo
cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Bw. Fahamu Mtulya.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora, Mhe. Salvatory Bongole (katikati) ambaye pia alikuwa Mhe. Mgeni rasmi wa Mafunzo hayo, akiwa
katika picha ya pamoja na Wanasheria wa Manispaa ya Tabora (waliosimama).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni