Na Rajabu Singana, Mahakama
Kuu Mbeya
Majaji wa Mahakama Kuu
waliohamishiwa Kanda ya Mbeya, Mhe. Robert Makaramba na Mhe. Paul Ngwembe
wamekaribishwa rasmi na watumishi pamoja na wadau wa Mahakama.
Waheshimiwa Majaji hao
walikaribishwa rasmi katika tafrija fupi iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika
ukumbi wa hoteli ya Usungilo jijini Mbeya.
Pamoja na kuwakaribisha
wageni tafrija hiyo pia ililenga kutambulisha Wadau muhimu wanaohusika katika
shughuli nzima ya utoaji haki ambapo ilisisitizwa kufanya kazi kwa ushirikiano
baina ya pande zote katika kutekeleza jukumu la utoaji haki.
Akifungua tafrija hiyo
mwishoni mwa wiki, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Dkt. Mary Levira kwa
aliwakaribisha Majaji wageni na kuwaelezea sifa mbalimbali za Mkoa wa Mbeya
kama vile wingi wa vyakula, ukarimu wa wenyeji pamoja na hali ya hewa nzuri.
Mara baada ya
kukaribishwa rasmi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Robert
Makaramba alipata fursa ya kuzungumza ambapo katika hotuba yake fupi aliwapongeza
Mahakimu wa Mahakama za mwanzo ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya kazi kwa
kujituma.
“Kazi ya Jaji au Hakimu sio kuamua tu bali
wana jukumu la kufundisha mawakili mahakamani, vilevile Wanasheria wa Serikali
na wa Kujitegemea pia wana jukumu kubwa katika utoaji haki kwa kuwa wanaweza
kuchelewesha au kupelekea haki kutolewa kwa wakati.,”. Aliongeza Mhe. Jaji Makaramba.
Naye, Mwenyekiti wa
Chama cha Mawakili Tanganyika tawi la Mbeya, Mhe. Joyce Kasebwa aliwakaribisha
Majaji hao na kuahidi kuwa Chama cha Mawakili kitaendelea kutoa ushirikiano kwa
viongozi hao ili kufanikisha jukumu kuu la Mhimili wa Mahakama la utoaji haki
kwa wakati.
Aliongeza kwa kusema Majaji
pamoja na Mahakimu wasisite kuwaelekeza na kuwafundisha Mawakili pale
wanapoonekana kwenda kinyume na matakwa ya sheria, kanuni na taratibu katika
uendeshaji wa shughuli za Mahakama.
Mhe. Jaji, Dkt. Mary Levira
akitoa neno katika ufunguzi wa tafrija ya kuwakaribisha rasmi Wahe. Majaji waliohamia katika Kanda hiyo.
Majaji wageni
(katikati), Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya na Mhe. Jaji Paul Ngwembe wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Mahakimu walioshiriki katika hafla hiyo.
(Picha na Rajab Singana, Mahakama Kuu, Mbeya)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni