Na
Lydia Churi-Mahakama Sengerema
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema Mahakama itaendeleza ushirikiano uliopo kati
yake na mihimili mingine ili kurahisisha suala la utoaji na upatikanaji wa haki
nchini.
Akizungumza na kamati
ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Sengerema ikiongozwa na mwenyekiti wake
ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Jaji Mkuu alisema Mahakama inapata nguvu
zaidi ya kutekeleza majukumu yake ya msingi pale inapopata ushirikiano kutoka mihimili
mingine yaani Bunge na Serikali.
Alisema endapo Mihimili
yote mitatu ya dola haitashirikiana ni wazi kuwa kazi ya utoaji na upatikanaji
wa haki itakuwa ni ngumu. Aliongeza kuwa mihimili hii imewekewa utaratibu wa
kutekeleza majukumu yake pasipo kuingiliana.
Aidha, Prof. Juma
aliipongeza Mahakama ya wilaya ya Sengerema pamoja na Ofisi ya Mkuu wa wilaya
ya Sengerema kwa kuwa na uhusiano wa karibu na ushirikiano kwenye utekelezaji
wa majukumu yao.
Akizungumzia kuhusu
rushwa na uvunjifu wa maadili, Jaji Mkuu alisema Mahakama ya Tanzania imeamua
kupiga vita rushwa na ukosefu wa maadili kwa watumishi wake ambapo pia alimtaka
Mkuu wa wilaya ya Sengerema kutosita kuwaita na watumishi wa Mahakama watakaopotoka
kwenye suala la rushwa na maadili.
Alisema Mahakama imeamua
kutoa nakala za hukumu bure pamoja na kuingia mkataba na shirika la Posta ili
kusambaza nakala hizo pamoja na nyaraka nyingine, kama hatua ya kupambana na vitendo
vya rushwa.
Naye Mkuu wa wilaya ya
Sengerema Bwana Emmanuel Kipole alisema mahusiano kati ya Serikali na Mahakama
kwenye wilaya yake ni mazuri kwani wamekuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana na
kuheshimiana bila kuingiliana majukumu.
Mkuu huyo wa wilaya pia
amemwomba Jaji Mkuu kuongeza idadi ya Mahakimu kwenye Mahakama ya wilaya kwa
kuwa hivi sasa Mahakama hiyo ina hakimu moja
ambaye haendani na idadi ya mashauri yaliyopo kwenye Mahakama ya wilaya.
Aidha Mkuu huyo wa
wilaya pia alisema kwa kurahisisha hudumu kwa wananchi, wilaya yake imetenga
eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 24,282 kwa ajili ya kujenga Mahakama, kituo
cha Polisi na Magereza.
Wakati huo huo, Ofisi
ya Takukuru wilaya ya Sengerema imetoa pongezi kwa Mahakama kwa kuanzisha program
maalum ya kuelimisha Umma kila siku ya Alhamis kuhusu taratibu za Mahakama kwani
program hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza malalamiko ya rushwa wilayani
humo.
Jaji Mkuu anaendelea na
ziara ya kikazi mkoani Mwanza ambapo leo alitembelea Mahakama ya wilaya ya
Sengerema pamoja na Mahakama za Mwanzo za Sima, Busisi, Buyagi na Mahakama ya
Mwanzo Sengerema mjini. Jaji Mkuu pia alimtembelea Mkuu wa wilaya ya Sengerema.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwasili katika wilaya ya Sengerema kuendelea na ziara ya kukagua kazi za Mahakama aliyoianza jana katika Mkoa wa Mwanza.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika wilaya ya Sengerema kuendelea na ziara ya kukagua kazi za Mahakama aliyoianza jana katika Mkoa wa Mwanza.
Mkuu wa wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole akizungumza wakati alipotembelewa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ofisini kwake leo.Wa kwanza kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mwanza Mhe. Sam Rumanyika na wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Sengerema Mhe. Monica Ndyekobora.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimuelezea Mkuu wa wilaya ya Sengerema, Mhe. Emmanuel Kipole kuhusu kitabu cha Mpango Mkakati wa Mahakama kabla ya kumkabidhi.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisalimiana na watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Sengerema alipowasili katika wilaya hiyo leo kuendelea na ziara ya kukagua kazi za Mahakama aliyoianza jana katika Mkoa wa Mwanza.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Bwn. Samson Mashalla (wa pili kushoto) akifuatilia jambo wakati wa ziara ya Jaji Mkuu wilayani Sengerema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni