Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka wanafunzi kuwa na maadili mema, kufuata sheria na taratibu za nchi na kuachana na matendo yote yanayokiuka maadili ikiwemo wizi wa mitihani.
Akizungumza na
wanafunzi wa shule ya sekondari ya Nyampulukano iliyopo wilayani Sengerema
mkoani Mwanza, Jaji Mkuu aliwaambia wanafunzi hao kuwa wizi wa mitihani ni tatizo
la kwanza la ukosefu wa maadili katika jamii.
Aliwataka wanafunzi hao
kujenge tabia ya kujisomea mambo mbalimbali kwa kuwa karne hii ya ishirini na
moja ni karne ya sayansi na teknolojia yenye taarifa nyingi zitakazowasaidia kwa
maendeleo yao.
“Karne hii ya ishirini
na moja ni tofauti na karne ya ishirini, someni mambo mbalimbali ili mfahamu
nchi yenu inakwendaje”, alisema Jaji Mkuu huku akiwasisitiza waisome Dira ya
Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 ili wafahamu Tanzania itakuwa ni nchi ya namna gani.
Aidha, Jaji Mkuu pia
aliwashauri wanafunzi watakaopenda kuwa wanasheria hapo baadaye kuhakikisha
wanakuwa waadilifu katika jamii kwa kuwa fani ya sheria inahitaji mtu aliye na
maadili mema hasa na yule anayechukia na kuvipinga kwa nguvu zote vitendo vya
rushwa.
Hata hivyo alisema
kutokusoma sheria hakutawazuia kufahamu sheria mbalimbali za nchi na kuwa karne
hii ya ishirini na moja inahitaji fani zote kushirikiana ili kuwa na maendeleo.
Akizungumzia rushwa na
uchumi wa nchi, Jaji Mkuu alisema ziko nchi duniani zenye rasilimali nyingi na zimeweza
kubadili maisha ya raia wake na wakati huo huo zipo nchi zenye rasilimali
nyingi lakini hazijaweza kubadili maisha ya watu wake kutokana na rushwa hivyo
aliwataka wanafunzi hao kukataa rushwa kwa kuwa ni adui wa maendeleo yao.
Mahakama ya Tanzania
imeanzisha mpango wa kuzitembelea shule mbalimbali nchini kwa lengo la
kuwaandaa vijana kuwa na maadili mema katika jamii wakiwamo wanasheria wa
baadaye.
Jaji Mkuu anaendelea na
ziara yake ya kikazi katika mkoa wa Mwanza ambapo anakagua shughuli za mahakama
kwenye Mahakama zilizopo mkoani humo.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisalimiana na waalimu wa shule ya Sekondari Nyampulukano iliyopo Sengerema Mwanza alipowasili shuleni hapo kuzungumza na wananfunzi wa shule hiyo kuhusu suala la Maadili.
Sehemu ya wanafunzi wa shule ya Sekondari Nyampulukano iliyopo Sengerema Mwanza wakisubiri kumsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim
Hamis Juma.
Wanafunzi wa shule ya Sekondari Nyampulukano iliyopo Sengerema Mwanza wakisoma risala mbele ya Jaji Mkuu. Kupitia risala hiyo, Mahakama ya Tanzania imetoa kiasi cha shilingi milioni 3 kusaidia baadhi ya changamoto za shule hiyo. Sehemu ya wanafunzi wa shule ya Sekondari Nyampulukano iliyopo Sengerema Mwanza wakisubiri kumsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim
Hamis Juma.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa pamoja na watumishi wengine wa Mahakama ya Tanzania salipotembelea shule ya Sekondari Nyampulukano iliyopo Sengerema Mwanza. Wa tatu kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza Mhe. Sam Rumanyika na wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Emmanuel Kipole.
Waalimu wa shule ya Sekondari Nyampulukano wakimsikiliza Jaji Mkuu alipotembelea shule hiyo na wananfunzi wa shule kuhusu suala la Maadili. Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Nyampulukano iliyopo Sengerema Mwanza.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza Mhe. Sam Rumanyika akizungumza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni