Jumatatu, 15 Oktoba 2018

TATIZO LA VYOO MAHAKAMA ZA MWANZO KANDA YA SHINYANGA SASA KUWA HISTORIA


Na Emmanuel Oguda-Mahakama Kuu, Shinyanga

Mahakama Kanda ya Shinyanga imedhamiria kuhakikisha kuwa kila Mahakama ya Mwanzo inakuwa na vyoo bora ambavyo vitatoa huduma kwa Wananchi na wateja wa Mahakama pamoja na Watumishi wa Mahakama za Mwanzo waliopo katika Kanda hiyo. 

Akikagua baadhi ya Mahakama ambazo tayari zimeanza kutekeleza agizo la ujenzi wa vyoo bora wakati wa ziara ya ukaguzi wa Mahakama mapema mwezi Oktoba, 2018, Jaji Mfawidhi-Mahakama Kuu, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Jaji Richard Kibella amepongeza Mahakama ambazo tayari zimetekeleza agizo ambalo alilitoa mwezi Julai, 2018. 

Mhe. Jaji Kibella aliagiza kwa mara nyingine kwa Mahakama ambazo bado kuanza kutekeleza agizo hilo kufikia mwezi Desemba, 2018. 

“Mahakama za Mwanzo zinahudumia Wananchi wengi hivyo ni vyema kila Mahakama kuhakikisha inatunza mazingira yake kwa kuwa na huduma ya vyoo bora ili wananchi waweze kujisitiri pindi wawapo Mahakamani,” alisisitiza Mhe. Jaji Kibella.

Mhe. Jaji Mfawidhi huyo aliongeza kuwa Mahakama zote za mwanzo zilizopo ndani ya Kanda ya Shinyanga zinatakiwa kuanza mara moja ujenzi wa vyoo ili kutimiza azma ya utunzaji bora wa mazingira sambamba na kutoa huduma kwa wananchi.

Mahakama za Mwanzo ambazo tayari zimetekeleza ujenzi wa vyoo ni pamoja na Mahakama ya Mwanzo Kilago, Mahakama ya Mwanzo Mpunze na Mahakama ya Mwanzo Ukune na zote za Wilayani Kahama. 


Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Richard Kibella (katikati) akikagua na kujionea hali ya choo.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni