Ijumaa, 9 Novemba 2018

MAHAKAMA KUU KANDA YA SUMBAWANGA YAWAAGA KITAALUMA MAJAJI WAKE WASTAAFU WAWILI


Na Mayanga Someke, Mahakama Kuu Sumbawanga

Mahakama kuu Kanda ya Sumbawanga imewaaga rasmi  Kitaaluma Majaji wawili wastaafu wa Kanda hiyo ambao  ni Mhe. Jaji Kakusulo Sambo na Mhe. Jaji Kassim Nyangarika.

Hafla ya kuwaaga kitaaluma ilifanyika mapema Novemba 08 katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Rukwa na kuhudhuriwa na Wahe. Majaji , wanasheria, Watumishi wa Mahakama Kanda ya Sumbawanga, Wanasheria wa Serikali, Mawakili  wa kujitegemea, Polisi, Magereza na Wananchi.

Katika hotuba zao,Wahe Majaji  hao Wastaafu waliwashukuru Viongozi wa Mahakama ya Tanzania na Watumishi wote wa Mahakama kwa ujumla kwa kushirikiana nao katika kipindi chote cha utumishi wao.

Kwa upande wake Mhe. Jaji Mstaafu Sambo aliwashukuru watumishi wa Mahakama kwa ushirikiano waliompa wakati wote wa utumishi wake. Alisema namnukuu “Ukimuona Nyani mzee jua amekwepa mishale mingi”.Alisisitiza kufanya kazi kwa ushirikiano na kwa weledi.

Mnamo mwezi Novemba, 2006, Mhe. Jaji Mstaafu Sambo aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Amelitumikia Taifa kwa muda mrefu katika ngazi mbalimbali hadi kufikia Mei, 1, 2016 alipohitimisha safari ya Utumishi wa Mahakama.

Kwa Upande wake Mh Jaji mstaafu Kasim Nyangarika alitoa shukrani za dhati kwa watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza na Mahakama ya Kuu divisheni ya Biashara alikofanyia kazi  kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu Sumbawanga. 

Katika utumishi wa umma Mh Jaji Mstaafu Nyangarika aliwahi fanya kazi katika shirika la zamani la Mawakili wa Serikali, Shirika la nyumba la Taifa kama mwanasheria mkuu wa shirika hilo na mnamo tarehe 26 May 2008 aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania hadi June 12, 2016 alipostaafu rasmi kwa mujibu wa sheria.

Kwa Mujibu wa taratibu za kimahakama Jaji anapostaafu hustaafishwa kwa kufanyika shauri maalumu ambalo ndio hasa huitimisha zoezi zima la kustaafu kwa mujibu wa sheria.

Majaji Wastaafu Mhe. Jaji Kakusulo Sambo (wa pili kushoto) na Mhe. Jaji Kassim Nyangarika (wa pili kulia) wakiwa kwenye picha ya pamoja na Wahe Majaji wa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga, katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Jaji David Mrango, wa kwanza kushoto ni Jaji Lilian Mashaka wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya  Rushwa na Uhujumu Uchumi na wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Jaji Adam Mambi.



Wahe Majaji Wastaafu na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania  wakiwa kwenye picha ya Pamoja na Wanasheria wa Serikali.
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni