Mahakama Kuu Kanda ya
Tanga imefanya kikao cha kusukuma mashauri (Case
flow Management Meeting) na kujadili mikakati mbalimbali ikiwemo namna bora
ya kuzuia mashauri kuwa mrundikano na kuondoa vikwazo visivyo vya lazima ili
kurahisisha uendeshwaji wa mashauri.
Akiongoza Kikao hicho Novemba
05, Mwenyekiti wa kikao ambaye pia ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Tanga,
Mhe. Amiri Mruma aliwataka Wadau kutoa ushirikiano wa kutosha katika
kufanikisha lengo lililopo mbele yao.
“Wito wangu kwa Wahe.
Majaji na Mahakimu wa Kanda hii ni kufanya vikao vya awali na Wadau (Pre – session meeting) ili kuweza
kujadili masuala mbalimbali hususani changamoto za Mashahidi ili kurahisisha
uendeshwaji wa mashauri pindi vikao vya Mahakama (Session) vitakapokuwa vinaendelea,”
alieleza Mhe. Mruma.
Akisoma taarifa katika
kikao hicho, Katibu wa kikao ambaye pia ni Naibu Msajili Mahakama Kuu, Kanda ya
Tanga, Mhe. Francis Kabwe alisema, tangu kuanza mwaka 2018 Mahakama Kuu Kanda
hiyo imefanikiwa kufanya vikao vitatu (3) vya kesi za mauaji (criminal
sessions) ambapo jumla ya mashauri 20 ya usikilizwaji wa awali (PH) yalipangwa
kusikilizwa.
Mhe. Kabwe alisema kati
ya mashauri hayo, jumla ya mashauri 12 yaliisha na mashauri 8 yalitolewa
maelekezo ya kupangwa katika vikao vijavyo ambapo kati ya mashauri 8, mashauri
6 pia yalimalizika.
Kwa upande wa mashauri
ya mrundikano, Mhe. Kabwe alisema, Mahakama Kuu Tanga ina mashauri 21 yenye
umri kati ya miezi 13 – 24 yakiwemo mashauri ya Mahakama ya kazi.
“Mashauri hayo 21yamewekewa
mkakati madhubuti wa kuyaondoa ili kuzuia mrundikano (Back stopping) ambapo
tayari kikao kimoja kimeshaanza kusikiliza mashauri hayo mbele ya Mhe. Jaji Mruma
na kutarajiwa kumaliza Novemba, 15, 2018,” alisema Mhe. Kabwe.
Aidha; Mhe. Kabwe
aliwaeleza wajumbe kuwa kikao kingine kitafanyika kuanzia Novemba 12 hadi
Novemba 15, 2018 mbele ya Mhe. Jaji Edson Mkasimongwa.
Wajumbe waliohudhuria
ni kutoka Ofisi ya mwanasheria wa Serikali, Mawakili wa kujitegemea, Polisi,
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), CMA na Taasisi ya kutoa
msaada wa kisheria (TAWLA).
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu Tanga, Mhe. Amiri Mruma (aliyesimama) akizungumza na Wadau
waliohudhuria katika kikao cha kusukuma mashauri.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Francis Kabwe akiwasilisha taarifa katika kikao hicho. Katikati ni Jaji
Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Amir Mruma, wa pili kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Tanga, Bw. Ahmed Ng’eni, wa kwanza kulia ni Kaimu Mwenyekiti chama cha Mawakili wa kujitegemea
(TLS – TANGA CHAPTER), Bi. Linda Lugano na Kushoto ni
Kaimu Mwanasheria
wa Serikali Mfawidhi Mkoa wa Tanga, Mhe. Shose
Naimani.
Pichani ni baadhi ya Wadau waliohudhuria
kwenye kikao.
(Stori na Picha kwa hisani ya
Amina Ahmad, Mahakama Kuu-Tanga)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni