Na Mary Gwera, Mahakama
Mahakama ya
Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imepanga
kuwa na Jukwaa la pamoja kujadili masuala ya msingi ya biashara yenye lengo la
kukuza uchumi wa Taifa.
Akizungumza na
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma Novemba 12, Mwenyekiti wa Bodi
ya TPSF, Bw. Salum Shamte alimshukuru Mhe. Jaji Mkuu kwa kukubali pendekezo la
kuwa na Jukwaa hilo.
“Jukwaa hili
ambalo tumependekeza kufanyika mara nne (4) kwa mwaka litasaidia TPSF na
Mahakama ya Tanzania kujadili changamoto kwani kuna Mashauri ya Kibiashara
ambayo kimsingi yakimalizwa mapema biashara zitaendelea na hatimaye uchumi
utakua,” alisema Bw. Shamte.
Mbali na Jukwaa,
Mwenyekiti huyo ambaye aliambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF pamoja na
Wajumbe wa Bodi wa Taasisi hiyo ambao walimtembelea Mhe. Jaji Mkuu kwa lengo la
kujitambulisha, aligusia pia juu ya ucheleweshaji wa baadhi ya Mashauri ya
Kibiashara Mahakamani.
“Napenda kupongeza
jitihada zinazofanywa na Mahakama katika kuendelea na maboresho ya huduma zake,
hata hivyo napenda kugusia baadhi ya mashauri ya biashara yanayochukua muda
mrefu, hivyo Mhe. Jaji Mkuu tunaomba uliangalie hili kwa jicho ya kipekee,”
alieleza Mwenyekiti huyo wa TPSF.
Kwa ujumla ujumbe
huo uligusia masuala kadhaa yote yakiwa na lengo la kuboresha na kukuza Sekta
ya biashara na uwekezaji nchini ambayo Mahakama pia ina mchango katika
kufanikisha hili.
Kwa upande wake
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliwahakikishia Wajumbe
hao juu ya kasi ya maboresho mbalimbali ambayo Mahakama inaendelea kufanya
mojawapo ikiwa ni matumizi ya TEHAMA.
“Kwa sasa,
Mahakama ya Tanzania ina baadhi ya mifumo mbalimbali inayofanya kazi, kama
Mfumo wa Utunzaji Takwimu kwa njia ya Kielektroniki (JSDS), ‘e-filling’ na
kadhalika, na mingine hivyo tunahitaji ushirikiano na Wadau katika kuhakikisha
kuwa Mahakama inatimiza jukumu lake la utoaji haki,” alieleza Mhe. Jaji Mkuu.
Mhe. Jaji Mkuu
alisema Mahakama ya Tanzania ipo tayari kuipitisha TPSF kuhusu mifumo hiyo
kuona jinsi gani inafanya kazi.
Aidha; Mhe. Jaji
Mkuu aliutoa hofu ujumbe huo juu ya kasi ya Mahakama katika kushughulikia
mashauri yanayoletwa Mahakamani huku akieleza juu ya Mikakati ya Mahakama
katika kukabiliana na mlundikano wa mashauri kwa kila ngazi ya Mahakama
huku akitoa wito kwa Mawakili na Wadau wengine wa Mahakama kuendana sambasamba
na kasi hiyo.
Katika kuhakikisha
kuwa Mahakama inafikia malengo ya kumaliza mlundikano imejiwekea mikakati
mbalimbali ikiwemo kupanga muda wa kumaliza kesi kwa kila ngazi ya Mahakama.
Kwa upande wa
Mahakama za Mwanzo kesi zisizidi miezi sita (6), Mahakama za Wilaya/Mkoa
kesi zisizidi mwaka mmoja na kwa upande wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu
kesi zisizidi umri wa miaka miwili (2).
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (pichani) akizungumza na Ujumbe kutoka TPSF na
Viongozi wa Mahakama (hawapo pichani) ofisini kwake, Mahakama ya Rufani (T)
jijini Dar es Salaam.
Wajumbe wakimsikiza
Mhe. Jaji Mkuu.
Mwenyekiti wa Bodi ya
TPSF, Bw. Salum Shamte (kushoto) akizungumza jambo, kulia ni Mkurugenzi
Mtendaji wa TPSF, Bw. Godfrey Simbeye.
Sehemu ya Wajumbe wa
Kikao wakifuatilia.
Jaji
Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akichangia jambo katika
Mazungumzo kati ya Mahakama ya Tanzania na TPSF. Katikati ni Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hussein Kattanga na kushoto ni Msajili Mkuu, Mahakama, Mhe. Katarina Revocati.
Mtendaji Mkuu, Mahakama
ya Tanzania, Mhe. Hussein Kattanga akizungumza jambo, kulia kwake ni Msajili
Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati.
Mtendaji Mkuu, Mahakama
ya Tanzania, Mhe. Hussein Kattanga (aliyenyoosha mkono) akiwaonesha Wajumbe kutoka TPSF Bango la
Mapambano dhidi ya rushwa lililoandaliwa na Mahakama ya Tanzania ikiwa ni moja
mikakati ya Mapambano dhidi ya Rushwa.
Jaji Mkuu wa Tanzania
(kushoto) akimkabidhi zawadi ya nakala za vitabu vya Mpango Mkakati wa miaka
mitano (5) wa Mahakama ya Tanzania kwa Mwenyekiti wa Bodi ya TPSF, Bw. Salum
Shamte.
(Picha na Mary Gwera,
Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni