Jumanne, 6 Novemba 2018

MAHAKAMA YA MFANO INAWEZEKANA TIMIZA WAJIBU WAKO; JAJI MZUNA


Na Catherine Francis, Mahakama Kuu Arusha
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Jaji Mosses Mzuna  amesema kuwa Mahakama  Kanda ya Arusha inaweza kuwa Mahakama  ya mfano ikiwa kila mtumishi wa Mahakama  hiyo atatimiza wajibu wake kikamilifu. 

Akizungumza katika kikao cha  Watumishi wa Mahakama  wa Arusha mwishoni mwa wiki, Jaji Mzuna alisisitiza kwa kuwaonya watumishi wenye tabia za uzembe kazini kuacha tabia hizo kwani husababisha kazi kutokutendeka kwa ufanisi. 

Mhe. Jaji Mzuna aliwasihi pia Viongozi kuwa na uratibu mzuri wa matumizi ya fedha kwani matumizi mabaya ya fedha hukwamisha shughuli za Kimahakama.

“Wakati sasa umebadilika hivyo kila Mtumishi akae atafakari utendaji wake wa kazi na kubadilika  kabla ya kuchukuliwa hatua kwa uzembe,” Alieleza Jaji Mfawidhi huyo.

Mhe. Jaji Mzuna aliendelea kusisitiza hilo kwa kunukuu usemi wa Jaji Mkuu Mstaafu , Mhe. Jaji Augustino Ramadhani usemao ‘Mjue Kamanda wako’ akimaanisha kuwa ni wajibu wa kila Mtumishi kujua ni aina gani ya kiongozi anayewaongoza kwani yeye hapendi uzembe na uvivu kazini hivyo yawapasa kubadilika kuendana na kasi yake ya kiutendaji.

Aidha Mhe. Jaji Mzuna aliwapongeza baadhi ya watumishi wa Mahakama wenye usikivu kwa viongozi wao na wanajituma kutelea wajibu wao kwa bidii huku akisisitiza  hilo kwa kusema ‘Excellence is not an accident but it is a process’ akimaanisha kuwa  ubora wa kazi hauji kama ajali bali ni mchakato.
  Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha- Mhe. Jaji Mosses Mzuna akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kanda ya Arusha (hawapo pichani).
      Baadhi ya watumishi wa Mahakama waliohudhuria kikao wakimsikiliza Mhe.Jaji Mfawidhi.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni