Na
Lydia Churi – Mahakama
Majaji watano kutoka
Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Watu wa China wameitembelea Mahakama ya Tanzania ili kujifunza namna
mfumo wa utoaji haki wa Tanzania unavyofanya kazi na pia kubadilishana uzoefu
kuhusu masuala yakisheria na utoaji haki.
Majaji hao kutoka jimbo
la Zhejiang la nchini China pia wameitembelea Mahakama ya Tanzania kwa lengo la
kujifunza zaidi na kubadilishana uzoefu hasa kuhusu adhabu zinazotolewa na
Mahakama kwa ajili ya kuirekebisha jamii.
Akizungumza na Majaji
hao, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati amewaambia kuwa
Mahakama ya Tanzania ni chombo huru kinachotekeleza majukumu yake kwa uhuru
pasipo kuingiliwa na Mihimili mingine.
Akizungumzia adhabu
zinazotolewa na Mahakama katika kuirekebisha jamii hasa zile za kifungo cha
nje, Msajili Mkuu alisema adhabu hizo hutolewa kwa mujibu wa sheria na kwa
vigezo mbalimbali ikiwemo kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani na
kufanya shughuli za uzalishaji ili kuisaidia jamii.
Alisema Mahakama ya
Tanzania imekuwa ikishauri matumizi ya adhabu mbadala ikiwemo kazi za nje
badala ya adhabu za kifungo gerezani. Kupitia adhabu hizi, wafungwa watatumika
pia kufanya kazi za uzalishaji mali na kuisaidia jamii.
Kwa upande wao, Majaji
hao kutoka nchini China wamesema wamefika nchini kujifunza mfumo wa utoaji haki
unavyofanya kazi na hasa kuhusu adhabu zinazotolewa na Mahakama katika
kuirekebisha jamii kwa kuwa mfumo huo pia hutumiwa na Mahakama zao.
Kwa mujibu wa Majaji
hao, China inazo fursa nyingi za kuwaendeleza wanasheria kitaaluma na hivyo
wametoa wito kwa Mahakama ya Tanzania kutumia fursa hizo katika kuwaendeleza
watumishi wake kama ambavyo nchi nyingine zimekuwa zikifanya.
Pichani ni Msajili
Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati (aliyeketi mbele) akiwa katika mazungumzo ya pamoja na Wahe. Majaji kutoka Mahakama Kuu
Zhejiang iliyopo nchini China walipotembelea Ofisi ya Mhe. Msajili
Mkuu, Novemba 16, 2018.
Msajili Mkuu Mahakama
ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati (kushoto) akimpatia zawaji mmoja wa Majaji
kutoka Mahakama Kuu Zhejiang nchini China.
Waheshimiwa Majaji
kutoka Mahakama Kuu Zhejiang nchini China wakiwa katika picha ya pamoja na
Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati (katikati), wa tatu
kulia ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Menejimenti ya Mashauri, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya na
wa kwanza kulia ni Mtaalamu Mwelekezi wa Mawasiliano-Mahakama ya Tanzania, Dkt.
Cosmas Mwaisobwa.
Waheshimiwa Majaji
kutoka Mahakama Kuu Zhejiang nchini China wakiwa katika picha ya pamoja
walipokuwa katika Ukumbi namba moja (1) wa Mahakama Kuu, Dar es Salaam.
(Picha na Mary Gwera-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni