Katika kusherehekea sikukuu ya Uhuru, Chuo
Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kimefanya Bonanza lililowashirikisha watumishi
Chuo hicho pamoja na Taasisi mbalimbali kwa lengo la kuleta hamasa ya kufanya
mazoezi ili kuimarisha afya ya mwili na akili.
Bonanza hilo lililoongozwa na Mkuu wa Idara ya Mafunzo
ya Kimahakama na Sheria Bi. Mwanabaraka Mnyukwa lilianza asubuhi kwa mchaka
mchaka (jogging) na kufuatiwa na mazoezi ya viungo ambapo kulikuwa na michuano mikali katika michezo mbalimbali
iliyoungurimishwa katika viwanja vya Chuoni hapo.
Akifungua mashindano
hayo, Mwanabaraka alisema kuwa mwaka huu mashindano yameboreshwa na kutoa fursa
kwa taasisi nyingine kualikwa kushiriki ikiwemo Jeshi la Polisi Lushoto,
Kampuni ya simu ya TTCL, Benki ya NMB, na Halmashauri ya mji Lushoto.
“Mwaka huu bonanza
limeboreshwa zaidi ndio maana tumeamua kuwashirikisha watumishi wenzetu kutoka
nje ya chuo, wanachuo na hata wanajumuiya inayotuzunguka” alisema Mwanabaraka.
Alisema Bonanza hili limetoa fursa adimu
kwa Watumishi, Wanachuo na wanajumuiya wanaokizunguka Chuo kukutana na
kushiriki kwa pamoja katika michezo.
Aidha, katika mashindano
hayo, Washiriki kutoka polisi Lushoto walitoa ushindani mkali dhidi ya wenyeji
wao IJA katika michezo mbalimbali iliyohudhurishwa viungani hapo ambapo katika
michezo wa kuvuta Kamba wanaume, timu ya IJA iliibuka kidedea dhidi ya
Polisi kwa seti 2 – 1, katika mchezo wa kukimbiza kuku IJA na Polisi walitoka
suluhu kwa jinsia zote mbili kwa kila moja kujipatia kuku mmoja mmoja.
Katika mchezo wa riadha
Bi. Catherine Macha wa IJA alinyakua nafasi ya kwanza na nafasi ya pili
kuchukuliwa na Bi. Ansila Isidory wa Polisi Lushoto. Kwa wanaume Bw. Daniel
Lussa wa IJA alishika nafasi ya pili nyuma ya Bw. John Gaudence wa Polisi.
Aliyetia fora katika
Bonanza hilo ni Bw. Noel Njau wa IJA aliyewashangaza watazamaji kwa kumaliza
sahani kubwa ya pilau huku akitafuna pilipili mbichi kwa muda wa dakika 2 huku
Bw. George Barnoba akishika nafasi ya pili wote kutoka IJA.
Michezo mingine ilikuwa
kama ifuatavyo; shindano la kukuna nazi ushindi ulinyakuliwa na Bi. Martha
Bukuku wa IJA akifuatiwa na Bw. Masoud Juma wa Polisi Lushoto, shindano la
kunywa lita 1.5 ya soda Bw. Masoud Juma wa Polisi Lushoto alinyakua ubingwa na
mchezo wa mpira wa meza (pool table) Polisi Lushoto walinyakua ushindi kwa
kushinda seti 2 – 1 ya IJA, mpira wa Pete (netball), mpira wa wavu (Volleyball), mpira wa kikapu (basketball) .
Bonanza: Bw. Noel Njau wa IJA akiwa kwenye shindano la kula sahani kubwa ya chakula aina ya pilau pamoja na kutafuna pilipili mbichi kwa dakika 2. Bwn. Njau aliibuka mshindi kwenye mashindano hayo.
Bonanza: Pichani Watumishi wakiendelea kukimbia huku wakiwa wamevaa magunia.
Bonanza: Timu ya Polisi Lushoto wakiwa wameibuka kidedea kwenye mchezo wa kufukuza kuku.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni