Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Mawakili nchini kuzingatia kanuni mpya
za maadili na kutoa huduma bora za uwakili ili waendelee kuaminika na kuaminiwa
na wananchi.
Akizungumza kwenye
sherehe za kuwakubali na kuwaapisha Mawakili, leo jijini Dar es salaam, Jaji
Mkuu amesema kanuni za maadili, nidhamu
na tabia njema za Mawakili tayari zimeshaanza kutumika mwaka huu. Lengo
likiwa ni kuwasaidia Mawakili waendelee kuaminiwa na kuaminika, na kubaki ndani
ya misingi ya maadili na huduma bora za uwakili.
Kwa mujibu wa Jaji
Mkuu, kanuni hizo zinawataka Mawakili wote kuwa waadilifu wakweli, na wanaofanya
kazi kwa kuheshimu misingi ya haki. Aliongeza kuwa endapo wakili yeyote atavunja
kanuni atachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kusimamishwa kufanya
kazi ya Uwakili.
Akifafanua kanuni hizo
Jaji Mkuu amesema baadhi ya makosa yanayoweza kusababisha Wakili Wakili
kuchukuliwa hatua za kinidhamu ni pamoja
na kushindwa kumpa mteja wake taarifa za masuala aliyoajiriwa kufanya,
kushindwa kutoa taarifa kwa mteja wake pale anapohitaji, na kushindwa kutoa
huduma kwa sababu ya ulevi au matumizi ya dawa za kulevya au pombe na kushindwa
kuchukua hatua muhimu za kimahakama kwa niaba ya mteja wake na hatimaye shauri kuchelewa
mahakamani.
Alisema ingawa elimu ya
mawakili kutoka shule za msingi, sekondari, vyuo na hata elimu ya sheria kwa
vitendo imejengwa katika misingi na maudhui ya karne ya 20 lakini Mawakili hao
hawana budi kutoa huduma zinazokidhi
ushindani na matarajio ya huduma za karne ya 21.
Akizungumzia umuhimu wa kazi ya Wakili, Jaji Mkuu amesema Wakili
anahitaji kuaminiwa na kuaminika ambapo maadili
mema na uwezo ni nguzo kwa ushindani wa huduma za kiwakili hasa katika karne ya
21. Alisema
huduma bora na ushindani stahiki kwa karne hii utawezekana tu endapo Mawakili watajiendeleza kitaaluma na kutumia mifumo
ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Amesema kwa kuzingatia
umuhimu wa sheria katika kila nchi, wakili ni kiongozi, mshauri, mtetezi na
msimamizi wa kila jambo linaloratibiwa na kusimamiwa na sheria, hivyo amewataka
watumie sheria kutatua na kumaliza migogoro, na kuweka mazingira ya ustawi wa
maendeleo ya wananchi.
Naye Mwanasheria Mkuu
wa Serikali Mhe. Prof. Adeladius Kilangi amewataka Mawakili wanaofanya kazi na
watakaoajiriwa serikalini kuzingatia sheria na taratibu za utumishi wa Umma kwa
kutokutenda makosa ya jinai.
Mwanasheria Mkuu wa
Serikali pia amewataka Mawakili wanapotekeleza wajibu wao kuzingatia maslahi ya
wateja wao badala ya kuweka mbele maslahi
binafsi. Kiongozi huyo pia amewataka Mawakili kujitafutia kipato chao kwa njia
zilizo halali.
Jaji Mkuu wa Tanzania
amewakubali na kuwaapisha wanasheria 909 kuwa Mawakili wapya wakiwemo Majaji, Naibu
Wasajili, Mahakimu, Maprofesa wa sheria, Maafisa Waandamizi wa Jeshi la
Wananchi na Jeshi la Polisi, Wahadhiri, Mapadri, Mashehe pamoja na Balozi
Mstaafu katika sherehe za 59 za Mawakili zilizofanyika kwenye viwanja vya Shule
ya Sheria jijini Dar es salaam. Sherehe hizo zilianza kufanyika rasmi mwaka
1986.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa na Majaji wengine wakati wa sherehe ya kuwakubali na kuwaapisha Mawakili wapya 909 zilizofanyika jana kwenye viwanja vya shule ya Sheria jijini Dar es salaam. Wa pili kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Eliezar Feleshi.
Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa sherehe ya kuwakubali na kuwaapisha Mawakili wapya 909 zilizofanyika jana kwenye viwanja vya shule ya Sheria jijini Dar es salaam.
Sehemu ya Mawakili 909 wakiwa sherehe hizo jana.
Sehemu ya Mawakili 909 wakiwa sherehe hizo jana.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza kwenye sherehe ya kuwakubali na kuwaapisha Mawakili wapya 909 jana jijini
Dar es salaam.
Dar es salaam.
Rais wa Tanganyika Law Society (TLS) Mhe. Fatma Karume akizungumza kwenye sherehe hizo jana jijini Dar es salaam.
Sehemu ya Mawakili 909 wakiwa sherehe hizo jana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni