Wasaidizi wa Kumbukumbu
wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga wamekumbushwa kufanya kazi kwa
kuzingatia maadili pamoja na kuipenda kazi yao kwa muda wote.
Hayo yamesemwa mwishoni
mwa wiki na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Kumbukumbu na Nyaraka za Mahakama ya
Tanzania Bw. Thomas Manyambula alipofika Shinganya na kufanya kikao cha pamoja na
Wasaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama Mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza na
Watumishi hao wa Mahakama, Bw. Manyambula aliwasisitiza Watumishi hao kuwa
makini na matumizi ya Mitandao ya Kijamii hususani katika suala la usambazaji
wa Nyaraka za kiofisi, utunzaji wa siri za Mahakama, kuhifadhi kwa usahihi
kumbukumbu zote za Mahakama pamoja na kuthamini kazi wanazozifanya.
Akizungumza wakati wa
kikao hicho, Naibu Msajili Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Mhe. Sekela Mwaiseje alimshukuru Mkurugenzi huyo wa nyaraka kwa kuwakumbusha watumishi
kutekeleza wajibu wao hasa katika uhifadhi wa nyaraka za Mahakama pamoja na
kupenda na kuithamini kazi za kuhudumia wananchi.
Naye Mtendaji wa
Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga Bw. Ernest Masanja aliwaasa watumishi wa
Mahakama kuzingatia yale yote waliyoelekezwa na Mkurugenzi wa Usimamizi wa
Nyaraka na Kumbukumbu za Mahakama ili kuleta ufanisi na tija katika suala zima
la utoaji haki kwa Wakati.
Mkurugenzi wa Usimamizi
wa Kumbukumbu na Nyaraka za Mahakama ya Tanzania Bw. Thomas Manyambula akizungumza na Watunza Kumbukumbu wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Shinyanga (hawapo Pichani).
Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Shinyanga (Watunza Kumbukumbu) wakimsikiliza Mkurugenzi wa Usimamizi wa Kumbukumbu na Nyaraka za Mahakama ya Tanzania Bw. Thomas Manyambula |
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Shinyanga Bw. Ernest Masanja akizungumza na Watumishi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni