Na Ibrahim Mdachi, Chuo cha
Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto
Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kimeitisha kongamano maalum
la wadau, kupitia na kutolea maoni mtaala wa mafunzo elekezi kwa Mawakili na Wanasheria
wa Sekta ya Umma.
Akizindua kongamano hilo jijini Dodoma, mwishoni mwa wiki iliyopita kwa niaba ya Katibu Mkuu,
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Mick Kiliba,
alisema kwa ujumla mafunzo yatakayotolewa
na IJA yanalenga kujenga uwezo kwa wanasheria wapya wa Serikali.
Bw. Kiliba alisema kuwa Mafunzo hayo yanalenga kujua mifumo ya
uendeshaji wa shughuli za kiserikali, uongozi na utumishi wa umma. Kwa lengo la
kuwaandaa waajiriwa wapya wa kada ya sheria kutoa utumishi ulio bora na
uliotukuka.
Alisema kuwa, matarajio ya Ofisi
ya Rais Menejimenti ya Utawala Bora kupitia Mafunzo haya ni kuona kila Mwanasheria
aliyeajiriwa katika Utumishi wa Umma anafahamu ipasavyo; majukumu yake ya kazi.
Aliongeza kuwa ni wajibu wa Mwanasheria kujua wajibu wake kama Mtumishi
wa Umma, Muundo wa Serikali na Utunzaji wa siri za Serikali hali kadhalika
kuiva kimaadili na kinidhamu.
“Itakumbukwa kuwa, waraka Na.5 wa mwaka 2011 wa Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, unaelekeza kutolewa kwa
mafunzo elekezi kwa Watumishi wapya katika Utumishi wa Umma,” alieleza.
Aidha, kongamano hili ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano
wa Chuo cha IJA wa 2018/19 - 2022/23 ambapo Chuo cha IJA kilishirikiana na
Wataalamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya Umma
kama vile Mahakama ya Tanzania na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Miongoni mwa masuala muhimu
yanayoangaziwa katika mtaala huo ni pamoja na kuwawezesha waajiriwa wapya
kuelewa namna ya kuendesha shughuli za serikali, kuelewa sheria, kanuni na
taratibu katika Utumishi wa Umma.
Chuo cha IJA kimekasimiwa madaraka ya kuandaa na kutoa mafunzo ya awali
na elekezi kwa waajiriwa wote wa kada ya sheria katika sekta ya Umma nchini.
Mgeni
Rasmi, Bw. Mick Kiliba akitoa hotuba yake, kulia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama-Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akiteta jambo na Mgeni rasmi (kushoto).
Mgeni rasmi (katikati) akiwa katika picha ya
pamoja na wawakilishi na waalikwa katika kongamano hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni