Jumatano, 5 Desemba 2018

MAHAKAMA YAANZA KUSIKILIZA KESI KWA MTANDAO

Na Magreth Kinabo-Mahakama ya Tanzania  

Mahakama ya Tanzania kwa mara ya kwanza imeanza kuendesha kesi kwa kutumia mfumo wa Mawasiliano kwa njia ya picha za video yaani ‘Video Conferencing’ kwa kutumia vitendea kazi vyake yenyewe kwa kumsikiliza shahidi akiwa nchini Ufaransa.

Kesi hiyo imesikilizwa leo katika kituo cha Mafunzo cha Mahakama ya Tanzania kilichopo Kisutu jijini Dar es Salam na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara Mhe. Lugano Mwandambo.

Hatua ya kuanza kusikilizwa kwa kesi kupitia mfumo huu ni hatua ya mafanikio katika Maboresho ya Utoaji wa Huduma za Mahakama kwa wakati na kwa viwango kumfikia mteja.
Kesi hiyo ya madai namba 6 ya mwaka 2017 iliyosikilizwa kwa njia  picha za video inayohusu mdai  ambaye ni kampuni ya Sogea Saton anayeidai zaidi ya shilingi bilioni 3.8 Bank of Africa.

Aidha kupitia mfumo huo wa Video Conferencing, shahidi huyo aliweza kutoa ushahidi wake mbele ya Jaji na Mawakili wa upande wa mdai ambao walikuwa ni Dilip Kesaria na Veronika Mwanajengwa, wakati mawakili wa upande wa utetezi walikuwa ni Peter Swai na Rosan Mwambo.  Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 2, mwakani.

Mahakama ya Tanzania imeamua kutumia Tehama ili kurahisisha utoaji wa haki kwa wakati na pia kuokoa muda na kupunguza gharama kwa wananchi wanaofika Mahakamani kutafuta haki zao.
Aidha, mfumo wa Mawasiliano kwa njia ya picha za video (Video Conferencing) ulioanza kutumiwa na Mahakama ya Tanzania katika kusikiliza mashauri Mahakamani tayari umefungwa katika Kituo cha Mafunzo cha Mahakama kilichopo Kisutu jijini Dar es Salaam na Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya.

Mpango uliopo ni kufunga Mfumo huu kwenye Mahakama Kuu zote nchini pamoja na chuo cha Uongozi wa Mahakama kilichopo Lushoto mkoani Tanga.
  Kesi ikiendeshwa kwa njia ya Mtandao- 'Video Conferencing' kwa mara ya kwanza katika kituo cha Mafunzo cha Mahakama ya Tanzania kilichopo Kisutu jijini Dar es salaam. Kulia pichani ni Shahidi  namba tatu , Stela  Janot akitoa ushahidi wake akiwa nchini Ufaransa.

  Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara Mhe.Lugano  Mwandambo  akiendesha kesi kwa njia ya Mtandao ‘Video Conferencing’ aliyekaa  mezani  (katikati amevaa tai )katika  Kituo cha Mafunzo cha Kisutu. Kushoto ni Makarani  wa Mahakama Martha Cosmas na Fortunata Barnabas.




    

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni