Jumanne, 11 Desemba 2018

WATUMISHI WATAKIWA KUWA NA MAADILI KUJENGA TASWIRA YA CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA LUSHOTO

Na Lydia Churi-Mahakama Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Prof. Ibrahim Hamisi Juma amewataka watumishi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kujiepusha na vitendo vya rushwa, utoro kazini na uzembe wa namna yoyote ile ili kujenga taswira nzuri ya chuo hicho.
 
Akizindua baraza la tatu la chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Jaji Mkuu amesema vitendo hivyo si tu kwamba vitakitia doa chuo hicho bali pia vitaitia doa Mahakama ya Tanzania, Utumishi wa Umma na taifa kwa ujumla.
Jaji Mkuu pia amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa bidii, ushirikiano na kuhakikisha kuwa kila mmoja anatekeleza wajibu wake ipasavyo.
“Ni matumaini yangu kuwa pamoja na kuhamasisha mambo yanayohusu haki za Mtanzania, mtasisitiza uhimizaji wa wajibu ambao kila mfanyakazi anao”, alisema Jaji Mkuu.
Alisema baraza la wafanyakazi ni chombo muhimu ambacho kimepewa nguvu ya kisheria ili kuwapa watumishi nafasi ya kushiriki katika maamuzi ya utekelezaji wa masuala mbalimbali yanayohusu utendaji na ufanisi wa Taasisi.
Aidha, Jaji Mkuu aliwataka watumishi hao kutumia Mpango Mkakati wao pamoja na ule wa Mahakama ya Tanzania katika kutafuta na kupata ufumbuzi wa changomoto mbalimbali zinazowakabili.
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu amekipongeza chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kuanza kutoa mafunzo ya pamoja kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo pamoja na wajumbe wa mabaraza ya kata katika kanda ya Tabora ambayo kwa kiasi kikubwa yatasaidia kuboresha utendaji wa kazi wa mabaraza ya kata na kupunguza migogoro.
  Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto Mhe. Jaji Dr. Paul Kihwelo akimkaribisha Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipowasili kwenye ukumbi wa Nyaraka mjini Dodoma kuzindua rasmi Baraza la tatu la Wafanyakazi la Chuo hicho.
 Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto Mhe. Jaji Dr. Paul Kihwelo akizungumza wakati wa uzinduzi wa Baraza la tatu la Wafanyakazi la Chuo hicho.
   Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Ignas Kitusi akizungumza wakati wa uzinduzi wa Baraza la tatu la Wafanyakazi la
Chuo hicho.
 
  Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizindua rasmi Baraza la tatu la wafanyakazi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto
 mjini Dodoma.

 
 Watumishi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma mara baada ya kuzindua Baraza la tatu la wafanyakazi wa Chuo hicho mjini Dodoma.
 
 
 
 
 
 



 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni