Jumanne, 11 Desemba 2018

JAJI MKUU ATOA WITO KWA VIONGOZI KUELIMISHA WANANCHI TARATIBU ZA UPATIKANAJI WA HAKI

Na Lydia Churi- Mahakama Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa wito kwa viongozi wa Mahakama, Serikali pamoja na Dini kuwaelimisha wananchi taratibu mbalimbali za upatikanaji wa haki.
Akizungumza na wakuu wa wilaya za Chemba na Kondoa mkoani Dodoma leo alipoanza ziara ya kikazi mkoani Dodoma, Jaji Mkuu amesema wananchi wengi hawafahamu taratibu za upatikanaji wa haki hivyo viongozi hao wanao wajibu wa kuwaelimisha kwa lugha ya upole wanapofika kwenye maeneo yao ya kazi.
Alisema kutokana na kutokufahamu taratibu za upatikanaji wa haki, wananchi wengine wamejikuta wakipoteza haki zao na wengine kutumia muda mwingi kushughulika na kesi ambazo thamani yake hailingani na muda na mali iliyotumika.
“Wengine hudhani kupata haki ni kushinda kesi hawajui kwenye kesi kuna kushinda na kushindwa, dhana hii ndiyo inayoibua migogoro hivyo wananchi hawana budi kuelimishwa kuwa haki kwa aliyeshindwa ni kukata rufaa”, alisema Jaji Mkuu.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania imejiwekea vigezo ili kuhakikisha inaboresha huduma zake na wananchi wanapata haki kwa wakati.
Vigezo hivyo ni pamoja na kuhakikisha kesi inamalizika ndani ya miaka miwili kwenye Mahakama Kuu, miezi 12 kwenye Mahakama za Hakimu Mkazi pamoja na Mahakama za Wilaya  na miezi sita kwenye Mahakama za Mwanzo.
Kigezo kingine ni mapambano dhidi ya rushwa ambapo alisema Mahakama imesambaza nchi nzima mabango yenye ujumbe wa mapambano dhidi ya rushwa, simu za mikononi na pia imewapatia watumishi wake wote vitambulisho.
Alisema Mahakama inaimarisha vitengo vya usuluhishi kikiwemo kitengo cha usuluhishi na mabaraza ya kata hasa kwenye maeneo  yasiyokuwa na Mahakama za Mwanzo.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Mahakama pia hutoa nakala za hukumu bure na kuhakikisha nakala hizo zinatoka ndani ya siku 21, kupatikana kwa mienedo ya kesi ndani ya siku 30 ili kuwafikia wananchi na kutoa haki kwa wakati.
Akizungumzia ushirikiano na mihimili mingine, Jaji Mkuu alisema mihimili yote ya dola inategemeana hivyo Mahakama haina budi kushirikiana ili wananchi wapate haki kwa wakati.
Naye Mkuu wa wilaya ya Chemba, Simon Odunga akimkaribisha Jaji Mkuu wilayani kwake alisema wilaya yake itaendeleza ushirikiano kati yake na Mahakama ya Tanzania.
Jaji Mkuu wa Tanzania ameanza ziara ya siku mbili katika mkoa wa Dodoma ambapo leo ametembelea wilaya ya Chemba pamoja na Mahakama ya wilaya ya Kondoa na kukagua shughuli za Mahakama.
 Mkuu wa wilaya ya Chemba, Simon Odunga akizungumza wakati Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipomtembelea ofisini kwake . Jaji Mkuu ameanza ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Dodoma ambapo atakagua shughuli za Mahakama.
  Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza wakati alipomtembelea Mkuu wa wilaya ya Chemba, Simon Odunga ofisini kwake .
 Mkuu wa wilaya ya Chemba, Simon Odunga akielezea jambo wakati akionyesha eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya wilaya kwenye wilaya yake . Wa kwanza kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Ignas Kitusi. 
 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimkabidhi Mkuu wa wilaya ya Kondoa Bibi Serazia Makota kitabu kinachoelezea Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania alipomtembelea Mkuu huyo wa wilaya
ofisini kwake.
 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisalimiana na Watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Kondoa alipowasili kuzungumza nao katika ziara yake ya kukagua shughuli za Mahakama.
  Mtendaji wa Mahakama kuu ya Tanzania Bwn. Leonard Magacha akifafanua jambo kwa watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Kondoa.
 Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Katarina Revocati akizungumza na watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Kondoa.
 Jengo la Mahakama ya wilaya ya Kondoa likiendelea kujengwa likiwa katika hatua za umaliziaji.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Kondoa Mhe. Francis Mhina akielezea jambo wakati Jaji Mkuu na ujumbe wake walipotembea jengo hilo linaloendelea kujengwa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni