Mahakama kuu ya
Tanzania, Divisheni ya Ardhi imefanikiwa kusikiliza na kumaliza mashauri 73
kati ya 92 yenye umri wa zaidi ya miaka mitano katika vikao Maalum (Sessions) viwili vilivyofanyika kuanzia Oktoba Mosi mpaka
Novemba 23, 2018.
Vikao hivyo maalum vya
kumaliza mashauri ya muda mrefu vilihusisha Majaji sita (6) wa Divisheni hiyo na
wengine watatu (3) kutoka nje ya Divisheni na kufanya idadi ya Majaji waliosikiliza
mashauri hayo kuwa tisa (9).
Kwa mujibu wa Taarifa
iliyotolewa kwenye kikao cha mwisho wa mwaka cha Divisheni hiyo kilichofanyika hivi
karibuni mashauri 73 kati ya 92 yaliyopangwa kusikilizwa yalisikilizwa na kutolewa
maamuzi ambayo ni sawa na aslimia 79.
Taarifa hiyo ilifafanua
kuwa mashauri 19 ambayo ni sawa na asilimia 21 ndiyo yaliyobaki na Majaji wanaendelea
kuyasikiliza nje ya utaratibu wa vikao (session) na wanakusudia kuyamaliza yote.
Katika kuhakikisha mashauri
yenye umri wa kuanzia miaka mitano na kuendelea yanaisha, Divisheni ya Ardhi pia
imeandaa kikao kingine cha tatu mbele ya Mhe. Jaji Amour Mohamed kilichoanza Novemba
26, 2018 kinacholenga kusikiliza na kutolea uamuzi mashauri sita (6) ambayo pia
yatamalizika. Kikao hicho maalum kinatarajiwa kukamilika Disemba 14 mwaka huu.
Kuhusu Mfumo wa
Uboreshaji wa Kumbukumbu za Mahakama (Judicial Statistical Dashboard System-
JSDS), Divisheni ya Ardhi imehamisha mashauri 3176 kutoka JSDS I kwenda JSDS II.
Hadi kufikia Disemba
12, 2018 Divisheni ilikuwa imehuisha mashauri 1474 na kusajili mashauri mapya
2707 kwenye mfumo wa JSDS II. Aidha, mashauri 1702 hayakuweza kuhuishwa kutokana
na changamoto za kimfumo na mashauri 378 kujirudia (Duplicate) ambapo suala hilo
linafanyiwa kazi.
Awali akifungua kikao hicho, Jaji Mfawidhi wa Divisheni
ya Ardhi aliwapongeza watumishi kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha ambao
umewezesha kutekeleza malengo yaliyowekwa na kuwaomba kuendeleza ushirikiano
huo.
Kikao cha kumaliza mwaka cha Divisheni kiliongozwa na
Jaji Mfawidhi Mhe. Rehema Kerefu na pia kuhudhuriwa na Majaji wengine wakiwemo Waheshimiwa
Leila Mgonya Salma Maghimbi na Awadh Mohamed. Kikao hicho pia kilihudhuriwa na
Mtendaji wa Mahakama, Naibu Msajili pamoja na Watumishi wengine.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi Mhe. Rehema
Kerefu akifungua kikao cha mwisho wa mwaka cha Divisheni ya Ardhi.
Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi wakiwa kwenye kikao hicho. Wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi wa Divisheni hiyo Mhe. Rehema Kerefu, wa Kwanza kulia ni Mhe. Salma Maghimbi. Wa kwanza kushoto ni Mhe. Awadh Mohamed akifuatiwa na Mhe. Leila Mgonya.
Baadhi ya Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi wakiwa kwenye kikao hicho.
Hongereni kwa kazi nzuri mliyoifanya kwa mwaka mzima
JibuFuta