Na
Mary Gwera, Mahakama-Morogoro
Mahakama ya Tanzania
inaendelea kutoa Mafunzo kwa Watumishi wake wa Kada mbalimbali ili kuwajengea
uwezo zaidi katika utendaji kazi na vilevile kwenda sambamba na kasi ya
maboresho ya utoaji huduma yanayoendelea kufanyika ndani ya Mhimili huo.
Akifungua Mafunzo ya Menejimenti ya Ununuzi na Usimamizi wa Mikataba
(Procurement and Contract Management PCM), yanayofanyika katika Ukumbi
wa Magadu Mkoani Morogoro mapema Januari 21, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa
Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo alisema kuwa Mafunzo hayo
ni muhimu kwani ni sehemu pia ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama.
“Mafunzo haya ni muhimu
katika kuboresha utendaji kazi, hatuwezi kuimba wimbo wa Maboresho Mahakamani
bila kuwawezesha Wataalam ambao wanachangia katika maboresho hayo,” alieleza Mhe.
Jaji Dkt. Kihwelo.
Aidha Mkuu huyo wa Chuo
alisema kuwa, Mafunzo hayo yanatolewa kwa Maafisa hao ikiwa suala la manunuzi
ni nyeti na linachukua nafasi kubwa katika utekelezaji wa Mradi wa Maboresho wa
huduma za Mahakama (CCP) ambapo kupitia mradi huo kuna ujenzi wa Mahakama
mbalimbali, ununuzi wa Vifaa vya TEHAMA na kadhalika.
“Vitu vingi vinahitaji
ununuzi, hivyo ni vyema Maafisa hawa na Wajumbe wa Bodi ya Zabuni kuongeza
ujuzi zaidi katika usimamizi wa mikataba inayohusiana na masuala ya ununuzi ili
kuepuka hoja zisizokuwa na msingi,” alisisitiza.
Kwa upande wake,
Mwezeshaji ambaye pia ni Mkufunzi kutoka chuo cha ESAMI-Arusha, Bw. Felix Kamau
alisema kuwa Mafunzo hayo yana faida kubwa kwani Washiriki wakifanya kazi kwa
kuzingatia taratibu za manunuzi kwa ufasaha itasaidia kuondoa hoja
zinazoibuliwa.
“Mbali na hilo, uandaaji
wa mikataba kwa usahihi, unawezesha pia kuondoa nyongeza za kazi ‘variations’
ambazo kwa asilimia kubwa huongeza gharama katika miradi mbalimbali hatimaye
Taasisi kuingia katika gharama zilizopo nje ya bajeti husika,” alieleza Bw.
Kamau.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni ya
Mahakama ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji-Mahakama ya
Tanzania, Bw. Mathias Mwangu alisema kuwa Mafunzo haya ni muhimu kwani asilimia kubwa ya Bajeti, kwa maana ya bajeti ya Matumizi,
ya kawaida na ya Maendeleo inahusisha Ununuzi.
“Hoja nyingi za Ukaguzi za
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zinatokana na udhaifu katika
menejimenti ya Mikataba, ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na taratibu za Ununuzi,
hivyo mafunzo yataongeza maarifa zaidi ya jinsi ya kukabiliana na mapungufu
hayo,” alieleza Bw. Mwangu.
Mafunzo hayo ya siku tano
(5) ambayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kupitia Chuo cha Uongozi wa
Mahakama kwa kushirikiana na ESAMI yamehusisha jumla ya Washiriki 40 kutoka
Kanda mbalimbali za Mahakama nchini.
Mkuu wa Chuo cha
Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo akizungumza
wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Menejimenti ya
Ununuzi na Usimamizi wa Mikataba (Procurement and Contract Management PCM).
Mwezeshaji
kutoka ESAMI, Bw. Felix Kamau akitoa Mada katika Mafunzo hayo.
Sehemu ya Washiriki wa
Mafunzo wakifuatilia kinachojiri katika Mafunzo hayo.
Mkufunzi kutoka Chuo
cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Bw. Lameck Samson Lushoto akizungumza
jambo katika Mafunzo hayo.
Washiriki
wa Mafunzo wakiwa kazi za vikundi ‘group discussions.’
Picha ya pamoja meza
kuu na baadhi ya Wajumbe wa Bodi: Katikati ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama
(IJA) Lushoto, Mhe. Jaji, Dkt. Paul Kihwelo, kushoto ni Mwezeshaji kutoka
ESAMI, Bw. Felix Kamau, kulia ni Mkurugenzi Msaidizi, Rasilimali Watu ambaye
pia ni Mjumbe wa Bodi ya Zabuni ya Mahakama, Bi. Agatha Ng’ingo, waliosimama
(katikati) ni Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni ya Mahakama, Bw. Mathias Mwangu,
kushoto ni Mjumbe wa Bodi, Mhe. Amir Msumi na kushoto ni Mjumbe wa Bodi, Mhe.
Warsha Ngh’umbu.
Picha ya pamoja, meza
Kuu, baadhi ya Wajumbe wa Bodi pamoja na Maafisa Ugavi wanaoshiriki katika Mafunzo hayo.
Maafisa hao wametoka Mahakama Kuu Masjala Kuu, Kanda ya Songea, Tanga, Arusha,
Dodoma, Iringa, Mwanza, Shinyanga na Divisheni zote za Mahakama Kuu ya Tanzania.
(Picha na Mary Gwera,
Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni