Na
Mary Gwera, Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Wasajili wa Mahakama nchini kuwa makini
katika usajili wa mashauri kwa kuzingatia taratibu za kisheria zilizopo ili
kuondokana na ucheleweshaji wa kesi hizo.
Akizungumza na
waandishi wa habari mapema Januari 25 mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa Mahakama
ya Rufani jijini Dar es Salaam, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa endapo kesi
zitasajiliwa bila kufuata taratibu za msingi ni dhahiri kuwa kesi husika zitaleta
changamoto katika mwenendo mzima wa usikilizaji kit kinachoweza kpelekea kesi
kufutwa na haki kupotea.
“Mahakama ni Mhimili
ambao upo wazi na unafanya kazi zake kwa kufuata taratibu na sheria zilizopo,
kwahiyo ni vyema kufuata taratibu hizo ili haki itendeke kwa wakati,” alisema
Mhe. Prof. Juma.
Mhe. Jaji Mkuu
aliyasema hayo alipokuwa akitoa taarifa kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na
Siku ya Sheria nchini kwa mwaka huu ambapo amewataka Wananchi ambao ndio Wadau
wakuu wa Mahakama kutembelea Maonesho yatakayofanyika kote nchini ili kupata
elimu ya Sheria.
“Katika kutimiza wajibu
wake wa Kikatiba wa kutoa haki, Mahakama imekuwa ikikumbana na changamoto
zinazohusiana na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu sheria na taratibu
zinazoongoza mashauri hivyo ni wito kwa wananchi wenye malalamiko/dukuduku
kutumia wiki hii kupata elimu badala ya kubeba mabango ya malalamiko kwenye
kilele cha siku ya Sheria,” alisema. Mhe.Jaji, Prof. Juma.
Mhe. Jaji Mkuu alisema
kuwa, kwa mwaka huu Maonesho ya Wiki ya Sheria nchini kwa upande wa Makao Makuu
ya Mahakama yatafanyika kitaifa mkoani Dodoma, na Kanda nyingine zitafanya
Maonesho hayo Kikanda.
“Maonesho ya utoaji wa
elimu ya sheria na shughuli za Mahakama kitaifa yatafanyika katika Viwanja vya
Nyerere ‘Square’ Jijini Dodoma kuanzia Januari 31, 2019 na kuhitimishwa na Siku
ya Sheria itakayofanyika Februari 06 jijini Dar es Salaam katika kiwanja cha
Mahakama, mtaa wa Chimala karibu na Hospitali ya ‘Ocean road’ kuanzia saa 03:00
asubuhi. Mhe. Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi,” alieleza Mhe. Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Jaji Mkuu alibainisha kuwa Maadhimisho
haya yanaashiria kuanza rasmi kwa mwaka mpya wa shughuli za Mahakama huku
Maudhui ya mwaka huu yakiwa ni “Utoaji wa Haki kwa wakati; Wajibu wa
Mahakama na Wadau.”
Aliongeza kuwa maudhui
haya yana maana kubwa kwa kuwa pamoja na jitihada zote za maboresho
zinazofanywa na Mahakama ni ukweli kuwa Mahakama haiwezi kutimiza wajibu wake
na kufikia Dira iliyojiwekea pasipokuwa na ushirikiano kutoka kwa Wananchi na
Wadau wengine wa Mahakama.
Mhe. Jaji Mkuu alisema
katika Wiki ya Sheria, Mahakama
itashirikiana na Wadau wake katika Sekta ya Sheria kutoa elimu juu ya taratibu
za ufunguaji wa mashauri, sheria na taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri, taratibu
za mashauri ya mirathi na ardhi, msaada wa kisheria, usikilizwaji wa malalamiko
na kadhalika.
Kwa upande mwingine,
Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa Wiki ya utoaji wa elimu ya sheria kitaifa
itazinduliwa rasmi jijini Dodoma Februari 02 kwa matembezi ya hisani yatakayoongozwa
na Mhe. Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa.
Pamoja na utoaji elimu
kwa umma, Mahakama itayatumia Maonesho ya Sheria kueleza hatua iliyofikiwa ya
utekelezaji wa Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (5) (2015/2016-2020/2021).
Maadhimisho ya Wiki ya
utoaji Elimu ya Sheria na Siku ya Sheria nchini huadhimishwa kila mwaka
kuashiria kuanza rasmi kwa shughuli za Mahakama kwa mwaka husika, kwa upande wa
Dar es Salaam Maonesho hayo yatafanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja kuanzia
Januari 31 hadi Februari 05, 2019.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani).
Msajili
wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. John Kahyoza (kushoto) na Mtendaji wa
Makhakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha (Kulia) wakimsikiliza Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipokuwa akizungumza na Waandishi wa
Habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu Maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria
nchini.
1.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akizungumza wakati wa Mkutano wa Jaji
Mkuu na Waandishi wa Habari kuhusu Maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria
nchini.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. Hussein Kattanga akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari wakati wa
mkutano kati yao na Jaji Mkuu wa Tanzania.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. Katarina Revocati akizungumza wakati wa Mkutano huo. Kulia ni
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi.
(Picha na Lydia Churi, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni