Na
Magreth Kinabo, Mahakama
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Majaji wapya
aliowaapisha kutenda haki kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza katika
hafla ya kuwaapisha Majaji hao iliyofanyika Januari 29, Ikulu jijini Dar es
Salaam, Mhe. Rais amesema kazi ya
kusimamia haki ni ngumu, hivyo inahitaji kumtanguliza Mwenyezi Mungu.
“Mna jukumu kubwa la
kusimamia haki, lakini mkamtangulize Mwenyezi Mungu, mkasimamie haki iliyo ya
kweli,” alisema Rais Magufuli.
Kwa upande wake Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
amempongeza na kumshukuru Mhe. Rais kwa kufanya uteuzi wenye idadi kubwa ya
wanawake.
Mhe. Samia alisema kwa
idadi hiyo ya Majaji wanawake anaamini masuala mbalimbali yaliyokubaliwa katika
Mkutano wa Arusha kuhusu Mahakama na Jinsia pamoja na ule wa Zanzibar wa Majaji
wanawake yatatekelezwa ipasavyo.
Awali kabla ya
kumkaribisha Mhe. Rais, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma
amesema uteuzi wa Majaji wapya umeongeza idadi yao kutoka 66 hadi kufikia
81.
Ametoa wito kwa Majaji
wapya kufanya kazi kwa bidii na unyenyekevu wa hali ya juu huku akiwataka
kujali na kulinda afya zao za mwili, akili na roho. Amesisitiza pia juu ya
utayari wao wa kufanya kazi kwenye kituo chochote cha kazi watakachopangiwa.
Aidha Mhe. Jaji Mkuu
ameonyesha kuwepo kwa hitaji la Majaji wengi Zaidi na kuainisha sababu za
hitaji hilo.
“ Bado upo umuhimu wa
Majaji kuongezeka hadi kufikia 100 au150 kwa kuwa uelewa wa haki umeongezeka na
wanachi wanaijua haki na wanakwenda Mahakamani na pia ujenzi wa majengo ya
Mahakama sehemu mbalimbali za nchi utaleta hitaji la kuwa na Majaji wengi
zaidi,” alisema Jaji Mkuu.
Katika hafla hiyo, Rais
Magufuli aliwaapisha Majaji sita wa
Mahakama ya Rufani, ambao ni Mhe. Winfrida Korosso, Mhe. Barke Sahel, Mhe.
Lugano Mwandambo, Mhe. Dkt. Mary Calorine Levira, Mhe. Ignas Kitusi na Mhe.
Rehema Sameji.
Rais pia amewaapisha
Majaji wa Mahakama Kuu, ambao ni Mhe. John Kahyoza , Mhe. Suzan Mkapa, Mhe.
Fahamu Mtulya, Mhe Cyprian Mkeha, Mhe.
Wilbard Mashauri, Mhe. Dustan Ndunguru,
Mhe. Seif Kulita, Mhe. Upendo
Madeha.
Wengine ni Mhe. Yohane
Masara, Mhe. Mustapha Ismail, Mhe.
Athman Kirati, Mhe. Zephrine Galeba, Mhe. Ntemi Kirikamajenga, Mhe.
Juliana Masabo na Mhe. Lilian Mongela.
Katika hafla hiyo
Majaji wapya, Wakuu wa Wilaya 2 na Wakurugenzi Watendaji wa Wilaya 10 walikula
kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa
umma.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
akimuapisha Mhe. Jaji Winifrida Korosso kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, kabla
ya uteuzi wake, Mhe. Jaji Korosso alikuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Divisheni
ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
akimuapisha Mhe. Jaji, Dkt. Mary Caroline Levira kuwa
Jaji wa Mahakama ya Rufani, kabla ya uteuzi huu Mhe. Jaji, Dkt. Levira alikuwa
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
akimuapisha Mhe. Ignas Kitusi kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, kabla ya uteuzi
huu, Mhe. Jaji Kitusi alikuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.
Mhe. Rais akimpongeza Mhe.
Jaji Kitusi mara baada ya kumuapisha.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
akimuapisha Mhe. John Kahyoza kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, kabla ya uteuzi wake,
Mhe. Kahyoza alikuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani (T).
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
akimuapisha Mhe. Suzan Mkapa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, kabla ya
uteuzi wake Mhe. Mkapa alikuwa Naibu Katibu Mkuu Hazina.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
akimuapisha Mhe. Upendo Madeha kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, kabla ya
uteuzi wake Mhe. Madeha alikuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi
Shinyanga.
Pichani ni Wahe. Majaji
Wateule wakisubiri kuapishwa rasmi.
Baadhi ya Waheshimiwa Majaji wa
Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu pamoja na Wageni wengine wakifuatilia
sherehe za kuapishwa kwa Wahe. Majaji wapya wa Mahakama hizo.
Wahe. Majaji wapya wa Mahakam
ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania wakila kiapo cha maadili mara ya
kuapishwa.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
akizungumza na Wahe. Majaji pamoja na Viongozi wengine aliowateua, katika
hotuba Mhe. Rais amewataka Viongozi hao kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na
taratibu zilizopo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.
Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Wahe. Majaji wapya walioapishwa,
amemshukuru Mhe. Rais kwa uteuzi wa Majaji hao.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wahe. Majaji wapya pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, wa tatu
kushoto ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu
Hassan, wa tatu kulia ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma,
wa pili kulia ni Katibu Mkuu Kiongozi, Eng. John Kijazi, wa pili kushoto ni
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, wa kwanza kushoto ni
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa ni Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), Mhe. Suleiman Jaffo na wa kwanza kulia ni Jaji Kiongozi, Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wapya walioapishwa na Majaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (katikati)
akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji Wakuu wa Mahakama ya Tanzania.
(Picha na Mary Gwera,
Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni