Na
Mary Gwera, Mahakama
Taasisi ya Slynn ya
nchini Uingereza imeahidi kushirikiana na Mahakama ya Tanzania katika masuala
mbalimbali ikiwemo kutoa Mafunzo kwa Waheshimiwa Majaji ili kuboresha huduma ya
utoaji haki nchini.
Akimzungumza na Jaji
Mkuu wa Tanzania mapema Januari 15, Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo
inayojishughulisha na masuala ya Haki, Bi. Alison Fenney alisema kuwa lengo la
ziara yao ni pamoja na kutaka kubaini maeneo ya ushirikiano.
“Lengo la kutembelea Mahakama
ya Tanzania ni pamoja na kujua taratibu mbalimbali za uendeshaji mashauri,
kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi na vilevile kuona jinsi gani Taasisi
inasaidia katika maeneo yatakayobainishwa,” alisema Bi. Fenney.
Katika msafara huo Bi.
Fenney aliambatana na Majaji Wastaafu, Mhe. Lord Bonomy na Mhe. Nic Madge pamoja
na Balozi wa Uingereza nchini, Bi. Sarah Catherine Cooke ambao kwa pamoja walifanya mazungumzo na Mhe. Jaji Mkuu
ofisini kwake Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na ugeni
huo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliainisha baadhi ya
changamoto ikiwa ni pamoja na baadhi ya wananchi kukosa huduma za Mahakama
katika maeneo waliopo au kusafiri umbali mrefu kupata huduma hiyo kutokana na
kukosa majengo.
“Tanzania ni nchi
kubwa, hivyo kuna baadhi ya maeneo ambayo wananchi hawapati huduma ya Mahakama
au hutakiwa kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hiyo,” alieleza Mhe. Jaji
Mkuu.
Aidha, Mhe. Jaji Mkuu
aliongeza kuwa, idadi ya Majaji ni ndogo ukilinganisha na wingi wa mashauri
yaliyopo ambapo alisema kuwa kila Jaji anasikiliza wastani wa kesi 400 kwa
mwaka kiwango ambacho ni kikubwa.
Kufuatia changamoto
hizi, Mhe. Jaji Mkuu alieleza kuwa Mahakama iliona ni vyema kuandaa Mpango
Mkakati ambao unatumika kama dira katika kutatua changamoto mbalimbali.
Aliongeza kuwa Mpango
Mkakati huo umejielekeza katika maeneo/nguzo kuu tatu (3) ambazo ni Utawala
bora, Uwajibikaji na Usimamizi wa Rasilimali, Upatikanaji
na utoaji haki kwa wakati na Kurejesha imani ya jamii na ushirikishwaji
wa Wadau.
Taasisi ya Slynn
iliyopo nchini Uingereza ina takribani umri wa miaka 30 inajihusisha na masuala
ya haki na sheria na inafanya kazi kwa
karibu na Majaji na Taasisi za haki duniani ili kuboresha mifumo ya utoaji haki
na uongozi wenye kufuata misingi ya sheria.
Ujumbe huo ambao
utafanya ziara ndani ya Mahakama kwa siku tatu umejielekeza kujua zaidi jinsi
gani Mahakama ya Tanzania inafanya katika suala zima la Usuluhishi ‘Mediation’ na
masuala mengineyo.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyeketi mbele) akizungumza na Ujumbe kutoka
Taasisi ya Slynn iliyopo nchini Uingereza, katika mazunguzo hayo walikuwepo pia
Viongozi Wakuu wa Mahakama; Mhe. Jaji Kiongozi, Mhe. Msajili Mkuu pamoja Naibu
Msajili Mwandamizi –Mahakama ya Rufaa.
Pichani ni Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisisitiza jambo katika mazungumzo
kati yake na ugeni uliomtembelea ofisini kwake.
Balozi wa Uingereza
Nchini Tanzania, Mhe. Sarah Catherine Cooke akizungumza jambo.
Jaji Mstaafu wa Mahakama
nchini Uingereza, Mhe. Lord Bonomy (kushoto) akiongea jambo. Katikati ni Balozi wa Uingereza nchini, Bi. Sarah Catherine Cooke, kulia ni Jaji Mstaafu wa Mahakama-Uingereza, Mhe. Jaji Nic Madge.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Juma (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na
Wageni na baadhi ya Maafisa wa Mahakama waliomtembele,
katikati ni Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu
ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi, wa nne kushoto ni Balozi wa Uingereza
nchini, Bi. Sarah Catherine Cooke, wa pili kushoto ni Jaji Mstaafu wa Mahakama
nchini Uingereza, Mhe. Jaji Lord Bonomy, wa nne kulia ni Jaji Mstaafu wa
Mahakama nchini Uingereza, Mhe. Jaji Nic Madge wa tatu kulia ni Mtendaji Mkuu
wa Taasisi ya Slynn, Bi. Alison Fenney, wa kwanza kushoto ni Msajili
Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati na wa kwanza kulia ni Naibu
Msajili Mwandamizi, Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Elizabeth Mkwizu.
Msajili Mkuu, Mahakama
ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati (wa nne kulia akiwaonesha Wageni kutoka
Taasisi ya Slynn, Ukumbi wa Kituo cha Mafunzo cha Mahakama kilichopo katika
eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Wageni hao walipata
nafasi ya kutembelea kituo hicho na kujionea ‘Video Conference’ iliyofungwa
katika kituo hicho, vilevile wageni hao walifanya mazungumzo na Jaji Kiongozi,
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.Dkt. Eliezer Feleshi.
(Picha na Mary Gwera,
Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni