Na
Ibrahim Mdachi, Chuo cha Uongozi wa Mahakama, Lushoto
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
(IJA) kimefungua mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo wa kanuni na mbinu za
usuluhishi Wajumbe wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar
(ZURA).
Mafunzo hayo ya siku tano yaliyoanza
mapema wiki hii, katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto mkoani Tanga,
yanaratibiwa na Mkuu wa Chuo hicho, Mhe. Jaji, Dkt. Paul Kihwelo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mhe.
Jaji Dkt Kihwelo alisema kuwa, mafunzo haya yamelenga kuwajengea uwezo wajumbe
wa Bodi na Viongozi wa ZURA ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi na kwamba
ana matumaini makubwa kuwa mara baada ya mafunzo haya washiriki watakuwa na
uelewa mpana zaidi wa kanuni na mbinu mbalimbali za usuluhishi.
“Chuo kimeandaa wakufunzi
waliobobea katika eneo la Usuluhishi ili kuipa ZURA mafunzo yatakayokidhi haya
na uhitaji katika utekelezaji wa majukumu yao,” alieleza Mkuu huo wa Chuo.
Mhe. Jaji Kihwelo alisema
kuwa wakufunzi hao wana uzoefu huku akiwataja kuwa ni pamoja na Mh. Jaji Mkuu
Mstaafu, Mohamed Chande Othman ambaye
ana uzoefu wa kutosha katika eneo la usuluhishi kwa ngazi ya kimataifa.
Wengine ni Mh. Jaji John Mroso (Jaji Mstaafu
wa Mahakama ya Rufaa) na Mh. Jaji Teemba (Jaji Mstaafu Mahakama Kuu) ambaye ni
mwanzilishi wa Kituo cha Usuluhishi nchini, akihudumu kama Jaji Mfawidhi wa
Kituo hicho.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu
Mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman alisema kuwa, lengo la kesi
kwenda kwenye usuluhishi ni kurudisha uhusiano mwema kati ya pande mbili zenye
mgogoro ili kuwawezesha kutatua mgogoro wao.
“Kuna
umuhimu wa mgogoro kusuluhishwa na wenye mgogoro wenyewe na sio mtu wa nje, na
ili usuluhishi ufanikiwe lazima wenye mgogoro waingie kwenye usuluhushi
wakiwa tayari kutoa na kupokea kwa sababu ukiingia huko suala la kushinda ama
kushindwa linawagusa wote tofauti na mahakamani ambapo mmoja hushinda na
mwingine hushindwa bila kusahau kuwa ni miongoni mwa njia za utatuzi wa
migogoro” alieleza Mhe. Jaji Mstaafu Chande.
Pia Jaji
Mkuu Mstaafu huyo alisema pia “sheria za nchi zetu mbili pamoja na katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara 107 (a) ibara ndogo 2 (d) inatamka katika
msingi wa utoaji haki ni kutatua migogoro kwa njia mbadala na ndio maana kwenye
mashauri ya kazi kuna njia mbadala za kwenda kwenye Mahakama za usuluhishi
(CMA).
Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Chande aliongeza
kuwa, “kwenye masuala la talaka na ndoa kabla hujaletewa mashauri mahakamani
lazima uende kwenye bodi ya usuluhishi na ni njia mbadala ya kuweza kutatua
migogoro hiyo kwa njia ya haki mtu kupata haki kwa sababu haki haipatikani Mahakamani
pekee.”
Kwa upande wake Jaji
Mstaafu wa Mahakama Kuu, Mhe. Jaji Rose Teemba
ambaye pia ni Mwanzilishi wa
kituo cha Usuluhishi nchini alisema kuwa kituo hicho kilianzishwa rasmi
kwa ajili ya mashauri ya madai yanayopelekwa Mahamakani kwa kutambua kwamba
sheria inataka usuluhishi ufanyike kabla ya shauri halijaingia kusikilizwa rasmi.
Hali hii ilipelekea Uongozi wa Mahakama
kuanzisha kituo hicho ili kuwe na wataalamu ambao ni Wahe. Majaji wataokuwa
wakifanya kazi hiyo ya usuluhishi kama kazi za kila siku kutokana na ukweli
kwamba Wahe. Majaji waliopo kwenye vituo vyao wamekuwa wakifanya kazi nyingi
kwa wakati mmoja.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) Bw. Ally Abood
Mzee Mjumbe alisema wao wamefarijika kupata fursa ya kuhudhuria mafunzo hayo na
wana matarajio makubwa kuwa watatoka wakiwa wameiva vyema katika eneo hili
muhimu na hivyo kuwawezesha kutatua migogoro iliyopo na itakayojitokeza kwa
weledi mkubwa.
Miongoni
katika faida za Usuluhishi ni pamoja na kusaidia kupunguza mlundikano wa
mashauri Mahakamani, kujenga mahusiano mazuri baina ya wadaawa na kupunguza
gharama za kesi za madai.
Mafunzo
haya kwa wajumbe wa Bodi na Viongozi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji
na Nishati Zanzibar (ZURA), ni mfululizo wa mafunzo ya namna hiyo kwa Mamlaka
ya Udhibiti wa Nishati, Maji na Mafuta, Tanzania Bara (EWURA) kuendeshwa na
Chuo cha IJA kwa mafanikio makubwa mnamo mwaka, 2017.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto na Mratibu wa mafunzo hayo, Mhe. Jaji Dkt. Paul F. Kihwelo
akizungumza wakati wa ufunguzi.
Jaji Mkuu Mstaafu na mwezeshaji Mkuu,
Mhe. Jaji Mohammed Chande Othman akieleza jambo wakati wa Ufunguzi.
Wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti
wa huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) wakiwa katika mafunzo ya
usuluhishi kwa vitendo mafunzoni. Nyuma ya ni Wawezeshaji wakifuatilia kwa
karibu zoezi hilo.
Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe.
Jaji Mohamed Chande Othman (aliyeketi katikati), Jaji Mstaafu wa Mahakama ya
Rufani, Mhe. Jaji John Mrosso (kushoto), Jaji Mstaafu Mahakama Kuu, Mh. Jaji Teemba
(kulia) na Mkuu wa Chuo, Mhe. Jaji Dkt. Paul F. Kihwelo (aliyesimama wa kwanza kulia)
wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za
Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) mara baada ya kufunguliwa rasmi kwa mafunzo.
Hongereni sana uongozi Mzima wa IJA kwa hatua kubwa. Mungu azidi kufanikisha mipango yenu. Ili wadau waweza kujijenga katika mbinu na kanunu za namna ya kutatua na kusuluhisha migogoro pasipo kwenda mahakamani.
JibuFuta