Ijumaa, 15 Februari 2019

JAJI AISHA NYERERE ASTAAFU: AWATAKA WATUMISHI KUWAPATIA WANANCHI HUDUMA ILIYOTUKUKA

Na Magreth Kinabo                                                                                                     

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi Mhe. Aisha Nyerere amestaafu Utumishi wa Mahakama na kuagwa rasmi na watumishi wa Divisheni hiyo ambapo amewataka watumishi hao kuendelea  kutoa huduma iliyotukuka kwa wananchi ili kuendelea kuipatia sifa Mahakama.

Akizungumza wakati wa hafla ya kumuaga iliyofanyika mwishoni mwa wiki, Jaji Nyerere aliyestaafu kwa mujibu wa kanuni  za  Utumishi  wa Umma aliwataka watumishi wa Divisheni hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano na kwa weledi huku wakiwa makini na watulivu wanapowahudumia wananchi.

“Endeleni kuipenda kazi na kuthamini utu na kuhakikisha  kila anayekuja kupata huduma Mahakama ya kazi anapata huduma  iliyotukuka” alisema  Jaji Nyerere.
Mhe . Nyerere pia aliwaasa Watumishi hao kujiepusha na vitendo vya rushwa ili wajenge taswira nzuri ya Mahakama kwa wananchi. Aidha aliwapongeza watumishi hao kwa kumpa ushirikiano alipokuwa akitekeleza majukumu yake kama Jaji na kuwataka kuendeleza ushirikiano huo kwa viongozi wengine wa Mahakama.
Naye Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Divisheni ya Kazi Mhe. Sophia  Wambura alimpongeza Jaji Nyerere kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi na upendo.“Tunaomba uendelee kutoa ushauri pale utakapohitajika,” alisema Mhe. Wambura.
Mhe. Jaji Aisha Nyerere alianza kazi rasmi mwezi Aprili mwaka 1984 ambapo aliajiriwa na Mahakama ya Tanzania kama Hakimu Mkazi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha.
Mwezi Novemba 28, 2006, aliteuliwa rasmi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.
Aidha, mwezi Julai mwaka 2010 hadi mwezi Mei, 2013 Mhe. Nyerere alikuwa ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha na Manyara ambapo kuanzia mwezi Mei 2013 hadi Desemba 2014 alikuwa ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Moshi.
Kuanzia Desemba 2014 hadi anastaafu, Jaji Nyerere alikuwa ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi. 
Nafasi nyingine alizowahi kushika Jaji Nyerere ni pamoja na kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Nyumba na Kodi katika Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro na Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Mikopo (LART TRIBUNAL) katika kipindi cha mwaka 2004-2005.

Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi wakiwa kwenye hafla ya kumuaga Jaji Mfawidhi wa Divisheni hiyo Mhe. Aisha Nyerere ambaye amestaafu kwa Mujibu wa Sheria.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi Mhe. Aisha Nyerere ambaye amestaafu utumishi kwa mujibu wa Sheria akizungumza wakati wa hafla ya kumuaga.

Jaji Mfawidhi Mstaafu Mhe. Aisha Nyerere  wa (pili kulia ) akiwa katika picha ya pamoja na  Majaji wenzake wa kwanza kulia ni Mhe. Jaji Zainab  Muruke, wa pili kushoto ni  Kaimu Jaji Mfawidhi  wa Mahakama Kuu Divisheni  ya Kazi Mhe.  Sophia  Wambura na wa kwanza kushoto ni  Mhe.Jaji Iman Aboud.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi Mhe. Sophia Wambura akimkabidhi Jaji Mfawidhi wa mahakama  hiyo Mstaafu Mhe. Aisha Nyerere zawadi ambayo ni kompyuta mpakato iliyotolewa na watumishi wa mahakama hiyo.

Jaji Mfawidhi Mstaafu,wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi Mhe.Aisha Nyerere(katikati) akitoa neno la kustaafu kabla ya kukabidhi kiti kwa Kaimu Jaji Mfawidhi  wa mahakama hiyoMhe.Sophia Wambura wa kwanza kulia, wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu  Divisheni  ya  Kazi Mhe. Iman  Aboud na watatu ni Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Zainab  Muruke.Kushoto wa kwanza ni Naibu Msajili Mfawidhi, Emmanuel Mrango, wa pili kushoto ni Naibu Msajili Safina Semfukwe na watatu kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Hellen Mkumbwa.

Jaji Mfawidhi Mstaafu, Mhe.Aisha Nyerere(kushoto) akimkabidhi vitendea kazi  Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi  Mhe. Sophia Wambura  (kulia) 

 

 








.

Maoni 2 :

  1. Madam Lady Justice Nyerere looks too young for retirement.

    JibuFuta
  2. Hongera sana Mhe. Jaji Aisha Nyerere kwa kumaliza kazi salama na ukiwa na moyo wa kuipenda Mahakama na Watumishi wake na kutuachia ujumbe mzito. Hakika tutauzingatia ujumbe huo. Mungu akubariki na akujalie afya njema.����

    JibuFuta