Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Prof. Ibrahim Hamis Juma leo amefungua mafunzo elekezi kwa Majaji kumi na watano (15) wa Mahakama Kuu ya Tanzania na kuwataka Majaji hao kuwajibika na kuzingatia Maadili na Uongozi bora.
Akifungua Mafunzo
elekezi ya Majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania leo katika kituo cha
Mafunzo kilichopo Kisutu jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu pia amewataka Majaji
hao kuzingatia matumizi ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano (Tehama) ili kurahisisha upatinaji wa haki.
Akizungumzia suala la
uongozi, Jaji Mkuu amewakumbusha Majaji wapya kutambua kuwa sasa wanao wajibu wa kiuongozi pamoja
na ule wa kazi zao za kila siku za kimahakama.
“Kama Viongozi,
mnapaswa sasa kufahamu mengi zaidi yanayoihusu Tanzania kwa ujumla pamoja na yale
yanayoihusu Mahakama ya Tanzania”, alisema.
Kuhusu uwajibikaji,
Jaji Mkuu amewataka Majaji wapya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili
ili kuimarisha na kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama. Alisema hakuna
Mahakama itakayosimama endapo wananchi watakosa imani na heshima dhidi yake.
Akizungumzia Matumizi
ya Tehama, Jaji Mkuu amesema matumizi ya Tehama ndani ya Mahakama siyo ndoto
tena kwa kuwa hivi sasa kazi nyingi zinafanywa kwa kutumia Tehama ikiwemo
kusajili Mashauri, kuhifadhi taarifa mbalimbali pamoja na kusikiliza mashauri.
Aliwataka Majaji hao kuhakikisha hawabaki nyuma katika matumizi hayo.
Kuhusu Maboresho ndani
ya Mahakama ya Tanzania, Prof. Juma amesema Majaji wapya wanayo bahati ya
kuingia ndani ya Mahakama wakati Mhimili huo ukitekeleza Mpango Mkakati wake wa
miaka mitano (2015/2016-2019/2020)
pamoja na Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama unaodhamiria kusogeza huduma
zake karibu zaidi na wananchi na kuwapatia haki kwa wakati.
Aidha, Jaji Mkuu pia
amewashauri Majaji wapya kuendelea kujiongezea ujuzi katika kazi zao. Alisema
Majaji bado wanahitaji elimu endelevu ya sheria ili waweze kutatua changamoto
za karne ya 21 pamoja na mabadiliko ya kasi ya ulimwengu wa sasa.
Naye Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania
Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi alisistiza umuhimu wa Majaji wapya kupatiwa Mafunzo
elekezi kwa kuwa mafunzo hayo ni endelevu na muhimu katika utekelezaji wa kazi yao.
Alisema kazi ya Jaji ni
ya kipekee hivyo inamtaka mtu kufuata maadili na kutenda haki wakati wote.
Akizungumzia Mafunzo
hayo, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto (IJA) Jaji Dkt.
Paul Kihwelo amesema katika mafunzo hayo, Majaji watapata fursa ya kujadili
changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo wakati wa kutekeleza wajibu wao,
kuzingatia maadili katika kutekeleza majukumu yao, pamoja na kukumbushana mifumo ya utendaji
kazi katika Mahakama ya Tanzania.
Amesema Majaji hao pia
watajadili namna mihimili mitatu ya dola inavyofanya kazi bila kuingiliana,
usuluhishi kwa njia ya muafaka na uandishi wa hukumu na utoaji wa adhabu.
Ni utamaduni wa
Mahakama ya Tanzania, kupitia chuo chake cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)
kuwapatia mafunzo elekezi nay a awali watendaji wake ili kuwaandaa kuwatumikia
wananchi kwa weledi na uadilifu.
Januari 27, mwaka huu,
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
aliwateua Majaji 15 wa Mahakama kuu ya Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni