Na
Lydia Churi- Mahakama, Dodoma
Watumishi wa Mahakama,
wadau pamoja na wananchi wametakiwa kila moja kutekeleza wajibu wake katika
mchakato uzima wa upatikanaji wa haki ili kesi ziweze kumalizika kwa wakati
Mahakamani.
Akizungumza kwenye
Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini kwa Mahakama Kuu kanda ya Dodoma, Jaji wa
Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo Mhe. Ignas Kitusi
alisema kesi kutokumalizika kwa wakati Mahakamani hakutokani na Mahakama pekee bali
wakati mwingine huchangiwa na wadau wa mahakama wakiwemo wananchi.
“Mawakili mnapaswa
kujiuliza pale mnaposhindwa kesi Mahakamani kwa sababu za kisheria, je mnawaeleza
wateja wenu ukweli kuwa mmeshindwa kutokana na makosa yenu au mnawaambia maneno
yanayoharibu sifa ya Jaji?” alisema Jaji Kitusi na kuongeza kuwa Mawakili nao
wana mchango katika kufanya kesi zisimalizike kwa wakati.
Kuhusu wananchi kwa
upande wao, Jaji Kitusi alisema wanao mchango mkubwa katika kukwamisha kesi
kusonga mbele pale wanaposhindwa kufika Mahakamani kutoa ushahidi katika kesi
mbalimbali. Aliwataka wananchi wanaotoa ushahidi Mahakamani kufanya hivyo kwa
kusema ukweli na kuwa na hofu ya Mungu.
Jaji Kitusi pia alitoa
wito kwa wananchi kuamini vyombo vya Sheria na pia kuwaamini Majaji na Mahakimu
wanapoendesha kesi zao ili haki zao zipatikane kwa wakati. Alisema kitendo cha
Mwananchi kutomwamini Jaji au Hakimu kinachangia kuchelewesha upatikanaji wa
haki.
Aidha, Jaji Mfawidhi aliwataka
wakuu wa Mikoa na wilaya nchini kuwashauri wananchi wanaopeleka malalamiko kwenye
ofisi za viongozi hao kuwashauri kutumia mfumo uliopo kisheria wa kukata rufaa
na si kulalamika ili kurahisisha upatikanaji wa haki.
Alitoa wito kwa jeshi la
Polisi nchini kuwaongezea uwezo askari wake wa upelelezi ili kesi ziendeshwe
kwa kutotegemea maelezo ya ungamo ya watuhumiwa kwa kuwa kwa kutumia maelezo
hayo huifanya kesi kuwa na ugumu inapofika mahakamani.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Binilith Mahenge aliipongeza
Mahakama ya Tanzania kwa Kauli mbiu ya mwaka huu ambayo alisema iko wazi kuhusu
suala la upatikanaji wa haki. Alisema upatikanaji wa haki kwa wakati hutegemea Mahakama, wadau na wananchi.
Alisema changamoto ya
upatikanaji wa haki kwa wakati iko kwa Watumishi wa Mahakama, Majaji na
Mahakimu pamoja na wananchi kwa kuwa kila mmoja ana changamoto zake katika
mchakato wa upatikanaji wa haki.
Naye
Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. John Samwel Malecela aliitaka Mahakama kutenda haki ili kudumisha Amani ya
nchi. Aliwataka viongozi wa Mahakama kutekeleza wajibu wao kwa kufuata haki na
utawala bora.
Maadhimisho ya wiki ya sheria
yalifanyika kitaifa katika jiji la Dodoma kuanzia Januari 31 na kufikiwa kilele
chake ambacho ni siku ya Sheria nchini Februari 6, 2019. Maadhimisho haya yamefanyika
nchini kotye katika ngazi ya Mahakama za wilaya na Mikoa.
Wanafunzi wa vyuo na shule za Sekondari pia walishiriki kwenye Maandamano ya kuadhimisha siku ya Sheria Nchini Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Ddodoma jana. Majaji wakiwa tayari kuanza shughuli za Maadhimisho mara baada ya Maandamano ya kuadhimisha siku ya Sheria Nchini Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Ddodoma jana. Katikati ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Dodoma Mhe. Ignas Kitusi. Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu kanda ya Dodoma Mhe. Latifa Mansoor na kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma Mhe. George Masaju.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Binilith Mahenge (katikati) akiongoza wageni mbalimbali walioalikwa kuhudhuria hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome.
Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Dodoma Mhe. Ignas Kitusi akijiandaa kukagua Gwaride la Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini.
Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Dodoma Mhe. Ignas Kitusi akikagua Gwaride la Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini.
Kikundi cha Ngoma ya Asili ya kabila la Wagogo wakitumbuiza wakati wa sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini.
Baadhi ya Mahakimu, watumishi wengine wa Mahakama ya Tanzania pamoja na wadau wakiwa kwenye sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini.
Baadhi ya Wanafunzi wakiwa kwenye sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini.
Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Dodoma Mhe. Ignas Kitusi akizungumza wakati wa sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni