Alhamisi, 28 Februari 2019

MAHAKAMA KUU KANDA YA SUMBAWANGA KUSIKILIZA JUMLA YA MASHAURI KUMI NA MBILI (12) YA MAUAJI


Na James Kapele  - Mahakama ya Hakimu Mkazi - Katavi

Jumla ya mashauri 12 ya Mauaji na mengine tisa (9) yamepangwa kusikilizwa katika ‘session’ maalum inayofanywa na Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga.

Vikao hivyo maalum vya Mahakama katika Kanda hiyo vitafanyikia Mkoani Katavi  kwa muda wa takribani mwezi mmoja (1) mbele ya  Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Mhe. David Mrango.  

Kazi hiyo muhimu ya  kusikiliza mashauri hayo yote ilianza Februari 25 na inatarajiwa kukamilika  Machi 22, 2019. 

Akizungumza na Wanahabari, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga, Mhe. Romuli Mbuya  aliwaeleza juu ya uwepo wa Kikao hicho na kwamba zoezi hilo la usikilizwaji wa mashauri ya aina hii  Mkoani Katavi ni endelevu na hufanyika mara kwa mara kutegemea na kukamilika kwa hatua zote za utayari wa kuanza usikilizwaji wa aina hiyo ya mashauri.

Kabla ya Kuanza kusikilizwa kwa Mashauri hayo Mhe. Jaji Mrango alikagua gwaride la heshima kuashiria ufunguzi rasmi wa mwaka wa Mahakama kwa kuwa kikao hicho ni cha kwanza kufanyika Mkoani Katavi baada ya siku ya sheria nchini kwa mwaka huu 2019.
 Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Sumbawanga, Mhe. David Mrango  akikagua gwaride la heshima kwa kuashiria ufunguzi rasmi wa Kikao cha Mahakama kuu Mkoani – Katavi.
Pichani ni baadhi ya watumishi wa Mahakama Mkoani Katavi na wadau mbalimbali waliohudhuria katika shughuli hiyo.
             

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni