Lydia Churi-Mahakama, Mtwara
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameagiza kupelekewa mashauri yote ya Mirathi nchi
nzima ili aweze kujua ni changamoto gani inayofanya yachelewe kumalizika na
kupanga mkakati wa kisheria ili mashauri hayo yawe yanaisha ndani ya muda
uliowekwa kisheria.
Akizungumza katika ziara
yake ya kikazi aliyoanza leo mkoani Mtwara, Jaji Mkuu alisema katika mahakama
za Mwanzo mashauri hayo yanatakiwa kwisha ndani ya miezi sita lakini yapo
mengine yamekaa zaidi ya miaka kumi.
Alisema kutokana na
kuchelewa kumalizika kwa mashauri haya, wakati mwingine humfanya msimamizi wa
mirathi kuendelea kunufaika na mali za marehemu wakati warithi wapo na
wanataabika kwa muda mrefu.
Jaji Mkuu amesema ametoa agizo
hilo pia kwa kuwa mashauri ya aina hiyo huweza kuzalisha migogoro mingi katika
jamii na kusababisha haki kutokupatikana kwa wakati.
Akizungumzia changamoto nyingine
zinazoikabili Mahakama ya Tanzania katika kutekeleza jukumu lake la msingi la
utoaji wa haki, Prof. Juma alisema Mahakama inakabiliwa na changamoto kubwa ya
wananchi kutofahamu taratibu za kisheria jambo linalosababisha washindwe kupata
haki kwa wakati.
Alisema hivi sasa
Mahakama ya Tanzania imejiwekea utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi juu ya
taratibu za kisheria kabla ya kesi kuanza kusikilizwa Mahakamani ili kuwasaidia
wanannchi kutambua nini cha kufanya.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu,
Mahakama imeamua kuwa wazi katika kutekeleza majukumu yake ikiwa ni moja ya
hatua muhimu za mapambano dhidi ya rushwa ndani ya Mhimili huo.
Awali akizungumza na Mkuu
wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa, Jaji Mkuu aliwaomba wakuu wa mikoa na
wakuu wa wilaya nchini kushirikiana na Mahakama ya Tanzania katika kuwaelimisha
wananchi taratibu za mchakato wa upatikanaji wa haki.
Alisema Mahakama
inachangia utulivu na Amani katika nchi pale inapotekeleza jukumu lake la
msingi la utoaji wa haki kwa wakati na endepo Mahakama haitafanya kazi yake
vizuri ni wazi itatoweka. Aliongeza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka
2025 pia imetoa mwelekeo wa Amani.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa akimkaribisha
Jaji Mkuu Ofisini kwake alisema Serikali kupitia Mkoa wake inashirikiana vizuri
na Mahakama katika kuwahudumia wananchi na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo.
Wakati
huo huo, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Bwn.
Solanus Nyimbi ili kutatua changamoto ya uchakavu na ukosefu wa miundombinu ya
Mahakama hususan majengo, Mhimili huo umeandaa Mpango Kabambe wa ujenzi
uliozingatia maeneo yanayotakiwa kujengwa majengo mapya ya Mahakama, pamoja na
yanayotakiwa kufanyiwa ukarabati mkubwa.
Alisema
hivi sasa majengo yanayoendelea kujengwa ni pamoja na Mahakama za Mwanzo 22,
Mahakama za Wilaya 20, Mahakama za Mikoa (Hakimu Mkazi) 8 pamoja na Mahakama
kuu 2, zinazojengwa katika mikoa ya Mara na Kigoma.
Alisema
wilaya ya Tandahimba nayo iko kwenye mpango wa kupatiwa jengo litakalojumuisha
mahakama ya Wilaya pamoja na Mahakama moja ya Mwanzo. Aliongeza kuwa lengo ni
kuwa na Mahakama katika kila makao makuu ya Tarafa.
Mtendaji wa Mahakama ya Rufani alisema ifikapo mwaka 2021 wilaya zote zisizo na majengo ya Mahakama
zitakuwa tayari zimepatiwa majengo hayo ambapo ujenzi huo utatumia fedda za
ndani pamoja na za Benki ya Dunia.
Jaji
Mkuu anaendelea na ziara yake ya kikazi aliyoianza leo katika mkoa wa Mtwara.
Alitembelea Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara pamoja na Mahakama ya
wilaya ya Tandahimba ambapo pia alipata fursa ya kuzungumza na watumishi.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisaini kitabu cha wageni alipowasili ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa kumsalimia ikiwa ni sehemu ya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Mtwara ambapo anakagua shughuli za Mahakama.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius
Byakanwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Mahakama Kitabu kinachohusu Maadili alipomtembelea ofisini kwake mara baada ya kuanza ziara ya kikazi katika Mkoa wa
Mtwara ambapo anakagua shughuli za Mahakama.
Mkuu wa Mkoa
wa Mtwara Mhe. Gelasius
Byakanwa akimkabidhi Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma zawadi ya Korosho kama alama ya kuwa mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa
wa Mtwara Mhe. Gelasius
Byakanwa akimwelezea jambo Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma. Kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara Mhe. Dkt. Fauz Twaib.
Watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Tandahimba wakimsikiliza Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipokuwa akizungumza nao alipokuwa kwenye Mahakama hiyo.
Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara wakimsalimia Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipowasili kuanza ziara kukagua shughuli za Mahakama.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Tandahimba Mhe. Sebastian Waryuba akizungumza wakati Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipomtembelea ofisini kwake. Kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Katarina Revocati.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni