Mahakama ya Tanzania imeanzisha
mpango wa kushirikiana na vyuo na shule za sekondari katika kuwalea na
kuwatambua wanafunzi wenye vipawa, tabia na maadili mema ambapo huwafuatilia na
kuwafanyia tathmini ili baadaye waje kufanya kazi na Mahakama pamoja na maeneo mengine
katika sekta ya Sheria
Katika wiki ya utoaji
wa elimu ya Sheria inayoendele jijini
Dodoma, wanafunzi kutoka baadhi ya vyuo vikuu na shule za sekondari nchini wanashiriki
kwa kujifunza masuala ya mbambali yanayohusu sheria pamoja na taratibu za
kimahakama jijini.
Akizungumza na Wanafunzi, Waalimu na Washauri wa wanafunzi
hao, kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Dodoma, Jaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Latifa Mansoor amesema kupitia Mpango huo wa Mahakama,
watumishi watakaoajiriwa na Mahakama ni wale tu wenye tabia na maadili mema na wenye
uwezo uliothibitika ili waweze kutoa huduma bora hapo baadaye.
Akizungumzia
utekelezaji wa mpango huo, Jaji Mansoor amesema baadhi ya mambo ambayo Mahakama
inashirikiana na vyuo na shule hizo ni kuwa na mahusiano ya karibu na kuwa na
fomu za ufuatiliaji wa mienendo ya maadili na taaluma za wanafunzi ambazo hujazwa
na kutumwa kwa Mahakama ya Tanzania mara mbili kwa mwaka.
Aliyataja mambo mengine
ya ushirikiano kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa klabu na utoaji wa elimu ya sheria mashuleni pamoja na
mpango wa kuwazawadia fursa za masomo na zawadi nyingine wanafunzi wenye vipaji
na maadili mema.
Aidha, Jaji Mansoor pia
aliwataka Waalimu na washauri wa shule hizo kuwalea na kuhakikisha kuwa wanafunzi hao wanakuwa na
ubora katika taaluma, tabia na maadili. Aliongeza kuwa wanafunzi wa vyuo hufuatiliwa
na kumbulkumbu zao huhifadhiwa kwa mahitaji ya baadaye ikiwemo ajira kwa
watumishi wa Mahakama na Sekta ya Sheria kwa ujumla.
Aliwataka wanafunzi hao
kusoma kwa bidii na kuwa na tabia na maadili mema kwa manufaa yao na ya taifa
kwa ujumla.” Tunawaalika katika maadhimisho haya ili kubadilishana uzoefu na
pia mjifunze masuala mbalimbali ya sheria ili muwe na ufahamu zaidi”, alisema.
Kufuatia Mpango huu wa
ushirikiano, Mahakama ya Tanzania inatarajia kuwa na huduma zilizoimarika,
watumishi kufanya kazi kwa ubora wa hali ya juu na kwa kuzingatia utawala wa
sheria, na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa maadili kupungua.
Vyuo ambavyo mpaka sasa
vimeingia kwenye ushirikiano na Mahakama ya Tanzania ni vyuo vikuu vya Dar es
salaam, Mzumbe, Dodoma, Ruaha, Iringa na chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Shule za sekondari ni
pamoja na Maua Seminari. Kisimiri, Shule ya Wavulana Ilboru, Shule ya sekondari
Kilakala, Shule za Sekondari za Wavulana za Feza, Marian na Tabora. Nyingine ni
Shule ya sekondari Msalato na Mazinde Juu.
Baadhi ya wanafunzi, Waalimu na Washauri wa wananfunzi wa Vyuo na Shule za
Sekondari wakiwa tayari kuzungumza na viongozi wa Mahakama leo jjini Dodoma.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Latifa Mansoor akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa Vyuo na Shule za Sekondari leo jjini Dodoma.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha, Justine Mlay akizungumza wakati wanafunzi wa Vyuo na Shule za Sekondari walipokutana na viongozi wa Mahakama leo jjini Dodoma.
Mwalimu wa shule ya Sekondari ya Wavulana ya Ilboru, Eliakim Singo akizungumza wakati wanafunzi wa Vyuo na Shule za Sekondari walipokutana na viongozi wa Mahakama leo jjini Dodoma. .
Mkurugenzi wa Utumishi na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania Bwn. Edward Nkembo akijibu maswali yaliyoulizwa na walimu, wanafunzi na washauri wa wanafunzi wa Vyuo na Shule za Sekondari walipokutana na viongozi wa Mahakama leo jjini Dodoma.
Mkurugenzi wa Ukaguzi na Huduma za Kimahakama wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Happiness Ndesamburo akijibu maswali yaliyoulizwa na walimu, wanafunzi na washauri wa wanafunzi wa Vyuo na Shule za Sekondari walipokutana na viongozi wa Mahakama leo jjini Dodoma.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma Mhe. Anold Karekiano akijibu maswali yaliyoulizwa na walimu, wanafunzi na washauri wa wanafunzi wa Vyuo na Shule za Sekondari walipokutana na viongozi wa Mahakama leo jjini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni