Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa
Kassim Majaliwa ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuanza kutoa huduma zake
kwa njia ya Tehama na kusema kuwa hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa haki
na kumpunguzia mwananchi mzigo wa kufuata huduma za mahakama.
Akizindua wiki ya
Sheria leo jijini Dodoma Waziri Mkuu amesema matumizi ya Tehama ndani ya
Mahakama ya Tanzania pia yatasaidia kuleta uwazi katika utoaji wa huduma na
kuwataka viongozi wa Mahakama kutokatishwa tamaa na changamoto za teknolojia zilizopo.
“Naunga mkono kwa dhati
uamuzi wa Mahakama ya Tanzania wa kutumia Tehama katika shughuli zake na
serikali ya awamu ya tano itafuatilia kwa karibu changamoto zitakazotokana na
matumizi ya Teknolojia kwa Mahakama na kuzipatia ufumbuzi”, alisema.
Akizungumzia Maonesho
ya Wiki ya Sheria, Mhe. Majaliwa aliwataka wananchi wa Dodoma kujitokeza kwa
wingi katika Maonesho hayo ili waweze kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu
upatikananji wa haki zao. Alisema wananchi wengi wana uelewa mdogo wa masuala
ya sheria na taratibu za kimahakama.
Aidha, Waziri Mkuu ameitaka
Mahakama ya Tanzania kuusambaza nchi nzima mfumo waliouanzisha wa kutoa elimu
ya Sheria kwa wanafunzi wa Shule za Sekondari na vyuo ili kuongeza uelewa wa
sheria kwa vijana na pia kuwajenga katika maadili yanayofaa.
Kuhusu kuwashirikisha
wadau katika shughuli zake, Waziri Mkuu amesema anavutiwa na Mahakama kwa hatua
ya kuwashirikisha wadau wake na kuwataka kuuendeleza ushitrikiano huo ili
wananchi wapate haki zao kwa wakati.
Naye
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
amesisitiza umuhimu wa Serikali kutumia ushauri wa kisheria wa Ofisi ya
Mwanasheria wa Serikali kwa kuwa hakuna
jambo lolote linalofanywa na serikali ambalo haliongozwi kwa sheria.
Alisema viongozi
wamekuwa wakitoa amri na maagizo yanayosababisha migongano ya kisheria na
hasara kwa Serikali hivyo ni muhimu kwa viongozi hao kufuata ushauri wa
wanasheria.
Aidha, Jaji Mkuu amewakumbusha viongozi wa
Serikali kuanzia ngazi ya vijiji, kata, tarafa, wilaya, mikoa, Idara na Wizara,
wabunge, Majaji, Mahakimu na watumishi wa Umma kuwa Mamlaka ya Mihimili mitatu
ya dola yanatokana na nguvu ya Sheria, na kuwa nguvu hiyo haimuonei mwananchi
yeyote”alisema.
Jaji Mkuu ametoa wito
kwa wakuu wa wilaya na mikoa ambao ni wenyeviti wa kamati za Maadili kwenye
wilaya na mikoa yao kujenga maadili na kuimarisha utawala wa sheria unaoheshimu nafasi pamoja na uhuru wa
Mahakama.
Alisema kutokana nafasi
zao katika kamati za Maadili, wakuu wa wilaya na mikoa wanayo nafasi ya kuomba
ushauri wa wanansheria wa Serikali kuhusu jambo lolote lililo kwenye himaya ya
Mahakama.
Alisema viongozi wa
ngazi mbalimbali wanapaswa kulinda na kusimamia Sheria za nchi ili kulinda
amani na utulivu katika nchi.
Kuhusu Maonesho ya wiki
ya sheria, Jaji Mkuu amewataka wananchi kutumia nafasi hiyo kujifunza na
kuelewa namna sheria zinavyofanya kazi, haki zao kisheria, taratibu za kudai
haki zao kwa mujibu wa sheria na maboresho yanayofanyika ndani ya Mahakama
yatakayosababisha sheria na mifumo ya
utoaji haki itumike kwa manufaa na ustawi wa wananchi.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa akiongoza Matembezi ya Uzinduzi wa Wiki na Siku ya Sheria nchini jijini Dodoma leo. Kulia kwake ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifuatiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Binnilith Mahenge anayefuatiwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula. Wa kwanza kushoto ni Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Tulia Akson
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa akiongoza Mazoezi ya viungo mara baada ya Matembezi ya Uzinduzi wa Wiki na Siku ya Sheria nchini jijini Dodoma leo.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa akipata Maelezo kutoka kwa Meneja wa kitengo cha Vinasaba (DNA) wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali bibi Hadija Mwema alipotembelea banda hilo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Hussein Kattanga akimuelezea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa kuhusu Maboresho ya huduma za Mahakama hususan ujenzi wa Miundombinu ya Majengo.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa akielezea jambo kuhusu Maboresho ya Mahakama alipotembelea banda la Kitengo cha Maboresho cha Mahakama.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa wiki ya Sheria. |
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki Matembezi ya uzinduzi wa wiki ya Sheria.
Brass Band ya Polisi ikiongoza Matembezi ya uzinduzi wa wiki ya Sheria.
Baadhi ya watumishi wa Mahakama pamoja na wadau wakishiriki Matembezi ya uzinduzi wa wiki ya Sheria.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni