Jumatano, 6 Februari 2019

RAIS MAGUFULI AIPONGEZA MAHAKAMA KWA MABORESHO: AZINDUA RASMI MAHAKAMA INAYOTEMBEA ‘MOBILE COURT’


Na Mary Gwera, Mahakama 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuanzisha huduma ya Mahakama inayotembea ‘mobile court’ kwani itasaidia kutoa haki kwa wananchi wengi zaidi.

Akizungumza katika sherehe za kilele cha Siku ya Sheria nchini, zilizofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais ambaye alikuwa mgeni rasmi katika shughuli hiyo, alisema kuwa amefurahishwa na huduma hiyo.

Aidha; Mhe. Rais, aliisifu Benki ya Dunia kwa ufadhili wa ununuzi wa Magari hayo ya Mahakama inayotembea ambayo ameyazindua huku akitaka idadi ya magari hayo kuongezwa ili kufikia maeneo mengi zaidi.

“Nakupongeza sana Mhe. Jaji Mkuu pamoja na Watumishi wote wa Mahakama kwa ujumla kwa maboresho ya Mahakama yaliyofanyika kwa mwaka jana, vilevile napongeza uanzishwaji wa huduma ya Mahakama inayotembea kwani itawasaidia wananchi kutatua migogoro mbalimbali” alieleza Mhe. Dkt. Magufuli.

Mahakama inayotembea, itaanza kufanya kazi katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza kwa kuzingatia wingi wa mashauri yanayofunguliwa katika mikoa hiyo, ambapo kwa Dar es Salaam huduma hii itatolewa maeneo ya Bunju, Kibamba, Chanika na Buza huku mkoani Mwanza huduma itatolewa; Buswelu, Igoma na Buhongwa.

Hata hivyo; Mhe. Rais aliitaka Mahakama kuelekeza huduma hiyo katika kutatua matatizo ya wananchi hususani wanawake wajane ambao wanahangaika muda mrefu kushughulikia mirathi.

“Maombi yangu, huduma hii iwasaidie pia wanawake ambao wengi wanahangaika kwa muda mrefu kushughulikia mirathi, ikibidi liwepo gari maalum ambalo ikiwezekana awekwe Jaji/Hakimu mwanamke kwa ajili ya kuwasaidia wamama wajane kuhusu masuala ya mirathi,” alisisitiza Mgeni rasmi.

Mbali na uzinduzi wa huduma ya Mahakama inayotembea, Mhe. Rais alizindua pia Mfumo wa kusajili na kuratibu mashauri (JSDS II).

Kwa upande mwingine; akizungumzia suala la maboresho ndani ya Mahakama, Mhe. Rais aliwataka wadau wote wa sheria kushirikiana na Mahakama ili kuwezesha mashauri kumalizika kwa haraka.

“Naomba niseme kuwa, maudhui ya Siku hii ya sheria kwa mwaka huu ni mazuri sana kwani yanamtaka kila mdau kushiriki katika huduma ya utoaji haki, hivyo ninawasihi Wapelelezi kujitahidi kufanya upelelezi kwa muda mfupi ili kuwezesha mashauri kumalizika kwa wakati,” alisisitiza Mhe. Rais.
Akitoa hotuba ya Siku ya Sheria nchini, naye Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alisema kuwa  hadi mwisho wa mwaka 2018, Mahakama za Mwanzo zilipokea jumla ya mashauri 176,652 na kumaliza mashauri 175,572 na kubakiza mashauri 15,675.

“Mahakama za Mwanzo kwa mwaka 2018 zilisajili asilimia 71.3 ya mashauri yote yaliyosajiliwa mahakamani ambayo ni mashauri 247,596. Hii inaonesha kuwa Mahakama za Mwanzo ndio hutumiwa zaidi na wanachi wengi wa kawaida mijini na vijijini,” alieleza Mhe. Jaji Mkuu.

Aidha; Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kuwa kati ya mashauri 15,675 yaliyobaki kwenye Mahakama za Mwanzo, ni mashauri 16 tu ndio yana umri zaidi ya miezi 6 (ili yaitwe mlundikano) ambao ni sawa na asilimia 0 ya mashauri yenye muda mrefu mahakamani yaani mlundikano.

Hata hivyo; Mhe. Jaji Mkuu alimhakikishia Mhe. Rais kuwa Mahakama ya Tanzania kupitia ngazi mbalimbali za mhimili huo imejipanga vilivyo kuhakikisha inamaliza mashauri kwa wakati stahiki.

Kwa upande mwingine, Mhe. Jaji Mkuu, Prof. Juma alimshukuru Mhe. Rais kwa kuongeza idadi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, na kuongeza kuwa bado kuna uhitaji wa Majaji kwa kuzingatia wingi wa mashauri yanayosajiliwa na wananchi.

Mahakama ya Tanzania, imekuwa katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini, kuanzia Januari 31 hadi Februari, 05 ambapo katika wiki hiyo, Mahakama mbalimbali nchini ziliadhimisha kwa maonesho maalum ya utoaji elimu ya sheria kwa wananchi na hatimaye kufikia kilele chake Februari 06, mwaka huu ambapo sherehe hizi huashiria uzinduzi rasmi wa mwaka mpya wa Mahakama.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (wa tatu kulia) pamoja na Viongozi wengine wakikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Mahakama inayotembea ‘mobile’. Wa tatu kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, wa pili kulia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai, wa kwanza kulia ni Waziri wa Katiba na Sheria,  Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, wa pili kushoto ni Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bi. Bella Bird na wa kwanza kushoto ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Sophia Mjema.

Mhe. Rais, Wahe. Majaji pamoja na Viongozi wengine wakiwa ndani ya gari ‘mobile court’ mara baada ya Mhe. Rais kulizindua rasmi, aliyeshika kipaza sauti ni Mkuu wa Idara ya TEHAMA, Bw. Enock Kalege, wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri, Mhe. Eva Nkya.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia Watumishi na Wageni waalikwa walioshiriki katika sherehe za Maadhimisho ya siku ya sheria nchini.
 
 Sehemu wa Watumishi na wageni mbalimbali waliohudhuria katika sherehe hizo.

Uzinduzi wa Mfumo wa kusajili na kuratibu mashauri (JSDS II).

Mhe. Rais akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi Wakuu wa Mahakama pamoja Viongozi wengine wa Sekta ya sheria.

 





Maoni 1 :