Na
Magreth Kinabo na Dennis Buyekwa
Mahakama ya Rufani ya
Tanzania kanda ya Mbeya na Dar es Salaam leo imesikiliza mashauri manne tofauti
kwa njia ya Mtandao (Video Conferencing) ambayo yamehusisha mashauri ya mauaji
na yale ya madai yote kutoka mkoani Mbeya.
Mashauri hayo yamesikilizwa katika Kituo cha Mafunzo kilichopo
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam huku Majaji wa Mahakama
hiyo wakiwa Dar es Salaam na washitakiwa
wakiwa Jijini Mbeya.
Shauri la kwanza linamhusu
askari mwenye namba E H/5842 D/C Maduhu
ambaye anadaiwa kukabiliwa na shitaka la
mauaji Katika kesi hiyo.
Katika shauri hilo
mtuhumiwa ameieleza Mahakama kuwa alishindwa kuwasilisha vielelezo vinavyotakiwa
na mahakama kwa sababu ya kutokuwa na mawasiliano mazuri baina yake na wakili
wake kitendo kilichopelekea mtuhumiwa kushindwa kupata vielelezo muhimu vilivyokuwa
kwa wakili wake. Maduhu aliwasilisha
maombi yake mbele ya Jaji wa Mahakama ya Rufani Mheshimiwa Rehema Mkuye.
Baada ya Wakili wa
Serikali kusikiliza maombi ya upande wa mtuhumiwa, Wakili wa serikali Rosemary
Mgeni alikubaliana na maombi hayo ya upande wa mtuhumiwa na kusema hana
pingamizi lolote dhidi ya mtuhumiwa.
Kufuatia hatua hiyo
Jaji wa Mahakama ya Rufani Mheshimiwa Mkuye ameomba kupewa muda ili akatafakari maombi hayo
na Mahakama itawapa taarifa juu ya uamuzi uliofikiwa.
Katika shauri jingine
la mauaji lililowakabili watuhumiwa wawili bwana Charles Kalungu na Charles
Kalinga, watuhumiwa wameiomba mahakama hiyo ya Rufani kuweza kuongezewa muda baada
ya kushindwa kuleta maombi yao ndani ya muda
uliopangwa wa siku 60 .
Baada ya wakili wa
Serikali kukagua viapo vya watuhumiwa na Mheshimiwa Jaji kujiridhisha kuwa
vinafanana, Mheshimiwa Jaji aliwaamuru watuhumiwa kuendelea na utetezi wao.
Wakitoa utetezi wao
mbele ya Jaji wa mahakama hiyo, Mheshimiwa Mkuye, watuhumiwa hao wameieleza
mahakama hiyo kuwa walishindwa kuwasilisha vielelezo hiyo kutokana na changamoto
mbali mbali walizokutana nazo katika ofisi za Idara ya Magereza, moja ya
changamoto iliyoelezwa na watuhumiwa hao ni kutokupata kiapo cha Afisa wa
Magereza kwa sababu Afisa huyo alishinndwa kuwasilisha kiapo hicho mbele ya
Jaji.
Kufuatia utetezi huo
Wakili wa Serikali Saraji Eboru, ameiomba mahakama hiyo kutoyakubali maombi
hayo kwa kuwa hayana sababu za msingi.
Baada ya Jaji wa Mahakama
ya Rufani Mheshimiwa Mkuye kusikiliza utetezi wa pande zote mbili
ameiomba mahakama hiyo kumpa muda ili akatafakari maombi hayo na mara baada ya
hapo atawajulisha uamuzi uliofikiwa.
Katika Shauri jingine
la madai lilimhusisha Oswadi Maruma dhidi ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya,
Oswadi ameiomba Mahakama ya Rufani mbele ya Mheshimiwa Jaji Sivangilwa Mwangesi
iweze kupitia upya shauri lake ili iweze kusikilizwa na Mahakama ya Rufani.
Wakili wa Serikali Hangi Chang’a ameiomba
Mahakama hiyo itupilie mbali shaurili hilo kwa kuwa halina msingi wa kuendelea
kusikilizwa na mahakama hiyo.
Baada ya Mheshimiwa
Jaji kusilikiza utetezi wa pande zote mbili ameomba apatiwe muda wa kwenda
kutafakari shauri hilo ili aweze kutoa uamuzi na aweze kupanga tarehe ya
kusikiliza shauri hilo.
Shauri jingine
limemhusisha Festo Sudi dhidi ya kijiji cha Iyombe, Wakili Simon Mwakolo kwa
niaba ya mteja wake ameiomba Serikali iweze kumuongezea muda mteja wake ili
aweze kuleta maombi ya kukata rufaa mahakama ya rufani nje ya muda wa siku
60 uliowekwa na mahakama hiyo.
Wakili huyo ameleta
maombi hayo kwa kuzingatia kanuni namba 4 (2a) cha mwaka 2009, kwa kuzingatia
shauri lililosikilizwa Mahakama kuu kanda ya Mbeya tarehe 24/10/1997, baada ya
shauri hilo kusikilizwa na kutolewa maamuzi
mlalamikaji aliomba shauri hilo liwe katika shauri namba 28 la mwaka
1997 ambapo maamuzi yake yalikataliwa tarehe 16/07/1999.
Mwaka 2000 mlalamikaji
alileta maombi mengine lakini Wakili wake wa wakati huo aliamua kuliondoa
shauri hilo Mahakamani pasipo kumshirikisha mteja wake.
Kufuatia hatua hiyo
mlalamikaji ameiomba mahakama hiyo iweze kumruhusu kuendelea na kesi hiyo kwa
kile alichoeleza kuwa kwa sasa ana uelewa juu ya madai ya msingi wa kesi hiyo.
Mheshimiwa Jaji Sivangilwa
Mwangesi baada ya kusikiliza upande wa mlalamikaji ameomba kupatiwa muda ili
aweza kutafakari maombi hayo kwa ajili ya kutoa maamuzi juu ya shauri hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni