Na
Mary Gwera, Mahakama
Ofisi ya Rais- Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) inashirikiana na Mahakama ya
Tanzania kupitia Mfumo wa Mahakama wa Kielektroniki wa Uratibu wa taarifa za
Mashauri (JSDS) ili waweze kupata taarifa za mashauri za Halmashauri mbalimbali
nchini.
Akizungumza katika
kikao cha kubadilishana uzoefu kati ya Mahakama na OR TAMISEMI kilichofanyika
Machi 26, 2019 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za Kitengo cha Maboresho
Mahakama (JDU), Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri, Mahakama ya
Tanzania- Mhe. Eva Nkya alisema ushirikiano huu umejikita katika eneo la
Kitehama.
“Ushirikiano wetu
umejikita katika eneo la Tehama ambapo, wenzetu wa TAMISEMI wamevutiwa na mfumo
wetu wa JSDS hivyo wamekuja kuangalia jinsi mfumo huu unavyofanya kazi na kuona
jinsi gani mfumo huu unaweza kuwekwa pia TAMISEMI,” alisema Mhe. Nkya.
Naye Mkurugenzi
Msaidizi wa Sheria, OR-TAMISEMI, Bw. Eustace Ngatale alisema kuwa andapo
wataunganishwa katika Mfumo huo utawasaidia kufahamu mzigo wa mashauri yaliyopo
kwa Halmashauri za Miji na za Wilaya.
“Mfumo huu pia
utatuwezesha kushughulikia changamoto mbalimbali na vilevile kujua aina ya
mashauri/kesi zinazokabili halmashauri mfano; mashauri ya mapato, mikataba,
ardhi, watumishi na kadhalika,” alieleza Bw. Ngatale.
Mkurugenzi huyo
aliongeza kuwa kupitia mfumo utawezesha kufuatilia na kufanya kazi kwa
kushirikiana na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kutimiza matakwa yote ili mashauri
yasikae muda mrefu.
Katika kikao hicho
Maafisa watatu kutoka OR-TAMISEMI ambao ni Mkurugenzi Msaidizi wa Sheria, Afisa
Sheria Mkuu na Afisa TEHAMA walipata nafasi ya kuwasilishiwa jinsi mfumo wa
JSDS unavyofanya kazi ambapo walionyesha kufurahishwa na mfumo huo.
Katika ushirikiano huu
Mahakama ya Tanzania na OR TAMISEMI watajenga mfumo shirikishi utakaowazeshesha
TAMISEMI kupata taarifa za mashauri yao kama ilivyoainishwa awali.
Kikao cha kubadilishana
uzoefu kati ya Mahakama na OR-TAMISEMI kikiendelea.
Mkurugenzi wa Usimamizi
wa Mashauri, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya akizungumza jambo katika kikao
hicho kati ya Mahakama na OR-TAMISEMI.
Mkurugenzi wa TEHAMA,
Mahakama ya Tanzania, Bw. Enock Kallege (katikati) akiwasilisha mada kwa ugeni
kutoka OR-TAMISEMI katika kikao cha kubadilishana uzoefu kilichofanyika katika
Ukumbi wa Ofisi za Kitengo cha Maboresho, Mahakama ya Tanzania (JDU).
Mkurugenzi Msaidizi wa
Sheria, OR-TAMISEMI, Bw. Eustace Ngatale (kushoto) akichangia jambo katika
kikao hicho, katikati ni Afisa Sheria Mkuu, OR-TAMISEMI, Bw. Merick Luvinga na
kulia ni Afisa TEHAMA, OR-TAMISEMI, Bw. Baraka Samson.
Afisa
Sheria Mkuu, OR-TAMISEMI, Bw. Merick Luvinga akichangia jambo.
(Picha na Mary Gwera,
Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni