Na Ibrahim Mdachi IJA -
Lushoto
Majaji wa Mahakama na Waendesha Mashtaka
kutoka nchini Ujerumani wapo nchini Tanzania kwa lengo la kubadilishana uzoefu na
Majaji pamoja na Waendesha Mashtaka wa Tanzania.
Akifungua Programu ya siku tano (5) iliyoanza
rasmi Machi, 25, 2019 Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Jaji
Moses Mzuna, katika hotuba yake aliwakaribisha wageni hao kwa niaba ya Mahakama
na kuwaeleza namna ambavyo Mahakama imefurahishwa na ujio wao na kwamba wana matarajio
makubwa ya kunufaika na programu hiyo.
Mhe. Jaji Mzuna alisema Programu hii inafanyika
ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kubadilishana uzoefu kati ya
Mahakama ya Ujerumani na Mahakama za Afrika (German and Africa Judiciaries
Exchange Programme).
Programu hii ambayo inatarajiwa
kumalizika Machi 29, 2019 inafanyika kwa mara ya kwanza Jijini Arusha katika
Ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Biashara ambapo washiriki kumi (10) wakiwemo Majaji
na Waendesha wameshiriki.
Naye, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha,
Mhe. Jaji Issa Maige mmoja wa washiriki aliwasilisha mada kuhusu mfumo wa sheria
na Mahakama nchini ikianzia Mahakama ya Mwanzo hadi ngazi ya Mahakama ya Rufani.
Vilevile alieleza jinsi gani Jaji wa Mahakama anavyopatikana sambamba na
utaratibu unaotumika.
Kwa upande wa Ujerumani Mhe. Jaji Evelyn
Oltmans Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Mjini Stuttgart huko Ujerumani alielezea
mfumo mzima wa kiutendaji wa Mahakama ya Ujerumani zikiwemo taratibu za kumpata
Jaji wa Mahakama ya Ujerumani, ambapo kupitia maelezo yake Majaji pamoja na
Waendesha Mashtaka wa Watanzania waliweza kujifunza na kuona utofauti ya ngazi
za Mahakama na pia hata jinsi Jaji anavyopatikana.
Mhe. Jaji Oltmans alieleza kuwa, kwa
upande wa Ujerumani Jaji anaweza akafanya kazi kwa muda na kisha kwenda kuwa
Mwendesha Mashtaka na baadaye kurudi tena kuwa Jaji kitu ambacho ni tofauti na
mfumo wa Tanzania.
“Si
Majaji wote wanaosikiliza mashauri ya jinai au madai, wapo Majaji maalumu
kulingana na aina ya mashauri, vilevile hata kwa upande wa Mawakili na
Waendesha Mashtaka wamegawanyika kwa utaratibu huo" alieleza Mhe. Oltmans.
Hali kadhalika, Mwendesha Mashtaka wa
Ujerumani, Dr. Eike Fesefeld aliwaelezea Washiriki juu ya taratibu na kanuni
zinazotumika katika kuendesha mashauri ya jinai ambapo alieleza kuwa kila jimbo
nchini Ujerumani lina katiba yake ambayo inatumika kuongoza uendeshwaji wa
mashauri lakini pia ipo katiba ya Jamhuri ya Ujerumani ambayo inatumika
kuongoza uendeshaji mashauri katika ngazi ya Mahakama ya Juu ‘Supreme Court’.
Katika kipindi watakachokuwepo nchini Majaji
hao watapata fursa ya kutembelea Mahakama Kuu kanda ya Mwanza na Arusha vile
vile Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama ya Afrika Mashariki pamoja na kusikiliza
mashauri katika mahakama hizo. Vile vile washiriki watapata wasaa wa kuambatana
na washiriki wenzao katika utendaji wa kazi wa kila siku.
Katika kutekeleza mpango huo,
inatazamiwa kuwa washiriki kutoka Tanzania watapata fursa pia ya kwenda Ujerumani
ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa zoezi hilo la ubadilishanaji uzoefu.
Programu hii imeandaliwa na Mahakama ya
Tanzania, Mahakama ya Ujerumani kwa ushirikiano na Mahakama ya Afrika Mashariki
na kuratibiwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda
ya Arusha ambaye pia ni Mgeni rasmi wa ufunguzi wa Programu hiyo, Mhe. Jaji Moses
Mzuna, akitoa hotuba fupi.
Mhe. Jaji Venerander Alexander
akitoa maelezo kuhusu mfumo wa utoaji elimu ya sheria nchini Ujerumani.
Hakimu Mfawidhi Mkoa wa Arusha, Mhe
Nikku Mwakatobe akiwaeleza jambo wageni hao.
Ujumbe wa Wawakilishi kutoka
Mahakama za Ujerumani na Tanzania katika picha ya pamoja na Wawakilishi kutoka Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni